MCHENGERWA AZINDUA MFUMO WA KADI JANJA ZA MWENDOKASI AWATAKA DART NA UDART KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA MAGARI. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

MCHENGERWA AZINDUA MFUMO WA KADI JANJA ZA MWENDOKASI AWATAKA DART NA UDART KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA MAGARI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa amesema SERIKALI imekuja na mwarobaini wa kudhibiti upotevu wa mapato katika mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa kuzindua mfumo wa kisasa wa kukusanya nauli kutumia kadi janja huku akitoa rai DART kwa kushirikiana na. UDART kuhakikisha inatatua changamoto ya uhaba wa mabasi yaendayo haraka kabla ya Desemba mwaka huu kwa kuwakaribisha Watanzania kushiriki katika zabuni kwa Dar es Salaam.

Sophia Kingimali.
By Sophia Kingimali.
02 Sep 2024
MCHENGERWA AZINDUA MFUMO WA KADI JANJA ZA MWENDOKASI AWATAKA DART NA UDART KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA MAGARI.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Septemba 2,2024 katika uzinduzi wa kadi janja na mageti katika mfumo wa DART, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa amesema mfumo huo utasaidia kuzuia udanganyifu na kuongeza mapato ya serikali huku akiagiza kadi hizo zianze kutumika mara moja.

Amesema uzinduzi huo unatokana na maendeleo ya teknolojia ya ukusanyaji wa nauli kwa DART,  ambayo inaufanya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kuwa katika kiwango cha juu kabisa.

“Niwapongeze DART kwa kutibu hoja za wananchi, uzinduzi wa kadi janja na kuachana na matumizi ya karatasi unaleta mapinduzi makubwa ya namna  tunavyotaka kuwahudumia Watanzania katika usafiri wa Dar es Salaam, inakwenda kujibu hoja na kutatua  changamoto za wananchi za kulipa nauli,

“ Ninatambua  hapo awali wananchi walipata changamoto nyingi , ukisoma katika mitandao ya kijamii, kila Mtanzania analalamika,  wapo waliokuwa wanalalamika kuhusu nauli zao, wapo waliokuwa wakitoa fedha zikiwa nyingi kupata chenji inachukua muda mrefu na wakati mwingine kukosa, sasa mfumo huu utajibu maswali yao ya muda mrefu,” amesema.

Aidha ameagiza upatikanaji wa kadi hizo kuwa rahisi bila changamoto  na DART kuongeza ufanisi kila anayetumia mwendo kasi afurahie kuishi Dar es Salaam, huku serikali ikijipanga kwenda katika majiji mengine pindi changamoto zote zikitatuliwa.

Mchengerwa amemtaka Mtendaji  wa DART na UDART kutekeleza suala la muda  wa mabasi kukaa kituoni na kuwa wakali  kwa watumishi wasiosikia  kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwahudumia Watanzania.

Amesema hatamani na hafurahishwi kuona watu wakikaa kituoni muda mrefu na wakati mwingine mabasi yakiwapita bila kuwachukua hivyo ameagiza changamoto hiyo itatuliwe haraka.

“Ni kweli kuna changamoto ya mabasi, Watanzania wanasubiri mabasi kwa njia ya Kimara  uhitaji ni mabasi 170  na Mbagala ni 500, DART hakikisheni mabasi yanapatikana  kabla ya Desemba, mwaka huu na muwakaribishe Watanzania  kushiriki zabuni kwa Dar es Salaam, waje kushirikiana na serikali katika uwekezaji,” amesema.

Aidha Mchengerwa amewataka watendaji hao zinapotokea changamoto zitatuliwe mara moja kwani hataki  kuona mabishano  katika masuala ya biashara, wasikae ofisini watoke kuwabaini wasiofanya kazi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Athuman Kihamia amesema mfumo wa kukusanya nauli wa kisasa wa kutumia kadi janja utasaidia kuepuka kutumia mfumo wa karatasi au keshi hali itakayopelekea utunzaji wa mazingira.

“Mfumo  huu uliojengwa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka  unafaida nyingi ikiwa kuondoa  matumizi ya karatasi yanayochangia uchafuzi wa mazingira.

“Pili kuondokana na suala la usumbufu katika chenji  kwani ukizingatia nauli sehemu nyingi ni sh.750, hiyo sh.50 imekuwa ikileta usumbufu  na muda mwingine haipatikani, pia hupunguza   muda wa kupanga  foleni kulipa  nauli katika vituo vyetu,” ameeleza.

Amesema kadi hizo zina ubora tofauti na  zinazotumia maeneo mengine kwani zina vitu vingi ambavyo mtu anaweza kutumia sio kulipa tu nauli.

VIONGOZI SOKO LA MACHINGA DODOMA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI

VIONGOZI SOKO LA MACHINGA DODOMA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI

BRELA YAWATAKA WASANIFU MAJENGO NA WAJASIRIAMALI KUTUMIA VIZURI BUNIFU ZAO.

BRELA YAWATAKA WASANIFU MAJENGO NA WAJASIRIAMALI KUTUMIA VIZURI BUNIFU ZAO.

MRAJISI VYAMA VYA USHIRIKA AGUSWA NA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO YA TTCL.

MRAJISI VYAMA VYA USHIRIKA AGUSWA NA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO YA TTCL.

MWENYEKITI WA BODI YA T-PESA AWATAKA WANANCHI KUWA WAZALENDO.

MWENYEKITI WA BODI YA T-PESA AWATAKA WANANCHI KUWA WAZALENDO.

PPAA YAOKOA BILIONI 567.6 KATIKA MICHAKATO YA ZABUNI ZA UMMA

PPAA YAOKOA BILIONI 567.6 KATIKA MICHAKATO YA ZABUNI ZA UMMA