Teknolojia ya 5G ya Airtel Kuleta Mageuzi ya Tehama Tanzania | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

Teknolojia ya 5G ya Airtel Kuleta Mageuzi ya Tehama Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa huduma ya mtandao inasambazwa kadri iwezekanavyo kwa watanzania wote vijijini na mijini ili kurahisisha matumizi ya teknolojia na shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Thobias Masalu
By Thobias Masalu
10 Aug 2023
Teknolojia ya 5G ya Airtel Kuleta Mageuzi ya Tehama Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa huduma ya mtandao inasambazwa kadri iwezekanavyo kwa watanzania wote vijijini na mijini ili kurahisisha matumizi ya teknolojia na shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Rais Samia ameyasema hayo August 10, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini wa 2Africa wa Kampuni ya Mtandao wa Simu ya Airtel pamoja na uzinduzi wa Teknolojia ya 5G ya Mtandao wa Airtel ambapo amesema kuwa ili kuhakikisha serikali inapunguza matumizi ya rasilimali fedha na kuongeza ufanisi haina budi kuruhusu na kuwezesha matumizi ya teknolojia ya habari (TEHAMA) katika maeneo mbalimbali ambapo shughuli za uzalishaji mali pamoja na za serikali zinafanyika.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Mkongo wa mawasiliano baharini wa 2Africa na Teknolojia ya 5G ya Kampuni ya simu ya Airtel 

Amesema kuwa ni lazima serikali iachane na matumizi ya nakala ngumu na badala yake kila kitu kifanyike kwa njia ya mtandao ili kurahisisha ufanisi na utendaji kazi katika sekta mbalimbali. 

“Leo tumezindua mkongo wa baharini na matumizi ya 5G, huduma za afya, elimu, utafiti kilimo zitaweza kupatikana kwa haraka zaidi hata kutoka nje ya nchi, teknolojia hii inaweza kutumika kwenye kilimo kwa kutumia drones (ndege nyuki) kupanda, kumwaga mbolea, kufukiza ama kuondosha wadudu lakini pia nimeona jinsi ya kuongeza matangazo ya utalii kwa kutumia teknolojia hii mtu aliyepo mbali anaweza kuiona Serengeti kwa kuvaa miwani ya aina yake, lakini pia nimeona teknolojia hii inavyotumika kwenye afya na kwenye maendeleo ya elimu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuzinduliwa kwa mkonga wa 2Africa kutatoa fursa kwa wananchi na watoa huduma wa mitandao mingine kuwa na uwanda mpana wa matumizi na machaguo, jambo ambalo linatarajiwa litaongeza ufanisi wa huduma na kupunguza gharama za mitandao kutokana na kuwepo kwa watoa huduma wengi kuliko ilivyokuwa hapo awali, aidha amesema katika kuzingatia mwelekeo wa maendeleo ya nchi katika uchumi wa kidigitali bado serikali ina safari ndefu na hivyo inatakiwa kuwepo kwa nguvu na jitihada zaidi ili kufikia malengo hayo.

Teknolojia ya Roboti lililotumika katika hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa mawasiliano baharini wa 2Africa na Teknolojia ya 5G ya Kampuni ya simu ya Airtel

“Serikalini kwetu bado hatujajipanga vizuri, matumizi ya mtandao huu bado hatujayatumia vizuri, naomba tujipange tufanye tathmini, tunahitaji kiasi gani kuziunganisha wizara na taasisi za serikali kutumia mitandao, kama ni mafunzo kwa watendaji hayo mafunzo yafanywe kwa watendaji, serikali iende kwenye mtandao tukifanya hivyo tutanusuru mambo mengi kwanza taarifa kupotea lakini pili ufanisi ndani ya taasisi za serikali utaongezeka, kwasababu tutajibizana kwa kutumia mtandao, hatuwezi kuimba kwenye majukwaa uchumi wa kidijitali kwenye ofisi zetu bado tuna njia za zamani.” Amesisitiza Rais Samia.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa watahakikisha wanayafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Rais Samia lakini pia kuendelea kuwavutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na wa nje ili kuongeza shughuli za uzalishaji mali ambazo zitaongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana wa kitanzania.

“Yote haya ambayo yamelengwa leo hii kuyafikisha kwa watanzania, yanatutaka tuwe na uelewa mkubwa wa namna serikali inavyohamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini, kwamba kuna mazingira mazuri ya uwekezaji tuko tayari kwa namna yoyote ambayo muwekezaji anahitaji kuhudumiwa na tunaendelea na pia tuwakaribishe wengine zaidi kuiga mfano wa Airtel kutuletea teknolojia mpya nchini.”

Rais Samia Suluhu Hassan akisilikiza maelezo kutoka kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye  wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa mawasiliano baharini wa 2Africa na Teknolojia ya 5G ya Kampuni ya simu ya Airtel 

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema serikali itahakikisha inatumia vyema Tehama ili kuhakikisha huduma mbalimbali zinafanyika kwa njia ya teknolojia, na itahakikisha kuwa huduma za mawasiliano nchini zinamfikia kila mtu, zinapatikana kila wakati, zinakuwa na bei inayoweza kutumiwa na watu wote, zenye ubora, usalama wa hali ya juu na zinabadili maisha ya watu.

“Mkongo wa 2Afrika una kasi ya terabyte 180 kwa sekunde mara kumi na moja zaidi ya ule tulionao, hili ni jambo kubwa kwa mustakabali wa nchi yetu, mkongo huu utaongeza kasi ya internet, ubora wa internet utaongezeka sana utasaidia katika jitihada za kushusha gharama za mawasiliano nchini, lakini pia ni fursa kubwa ya kuvutia uwekezaji wa kampuni kubwa duniani kama Google, Meta ambapo pamoja na kukuza uchumi wetu utatoa ajira kwa vijana wa kitanzania.” Amesema Waziri Nape.

Waziri Nape amesema matumizi ya Tehama kwa kutumia mkongo huo wa 2Africa, utarahisisha upatikanaji wa huduma za internet na kutolewa kwa huduma nafuu kwa watanzania.

“Mkongo huu na matumizi ya 5G nchini ni gamechanger kuelekea mainduzi ya nne ya viwanda yaani fourth industrial revolution Tehama ni njia kuu ya kufanya mapinduzi kwenye sekta zote nchini, umeona kwenye kilimo, afya, kwenye madini, kwenye utalii, elimu, utawala bora.” Amefafanua Waziri Nape.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa baharini 2Africa na Tekonolojia ya 5G ya Kampuni ya simu ya Airtel kwa njia ya Hologram

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airtel nchini Dinesh Balsingh amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwekeza kutokana na kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali ambayo yamekuwa kivutio kwa shughuli za biashara na uwekezaji lakini pia ameahidi ujenzi wa madarasa ya teknolojia (Smart classes) mia moja pamoja na kutoa huduma ya mtandao wa bure kwa jamii katika maeneo ambayo watayaainisha.

Uzinduzi wa mkongo wa baharini wa 2Africa ambao unatarajiwa kutumika katika mabara matatu ya Afrika, Asia na Ulaya una urefu wa kilomita 45000, utatumiwa na watu takribani bilioni 3 duniani kote na utaunganisha zaidi ya nchi thelathini, Mkongo huo umejengwa kwa ushirikiano wa Kampuni kama vile Meta inayomilki mitandao ya (Facebook, WhatsApp, Instagram, Thread), China Mobile, MTN ambapo kituo cha kutolea huduma kitaendeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania ambayo ina ubia na serikali.

Mfumo wa eMrejesho V2 umechaguliwa kuwania Tuzo za Dunia Jumuiya ya Tehama.

Mfumo wa eMrejesho V2 umechaguliwa kuwania Tuzo za Dunia Jumuiya ya Tehama.

WADAU WA UNUNUZI WAASWA KUZINGATIA MAADILI KAZINI

WADAU WA UNUNUZI WAASWA KUZINGATIA MAADILI KAZINI

TRA IMEWEZA Kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyabiashara Kujenga Mahusiano na Kutatua Changamoto.

TRA IMEWEZA Kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyabiashara Kujenga Mahusiano na Kutatua Changamoto.

Leseni 2,450 zatolewa na BoT kwa taasisi za mikopo daraja la pili

Leseni 2,450 zatolewa na BoT kwa taasisi za mikopo daraja la pili