Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027 | The Dodoma Post
The Dodoma Post Makala

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Joto la Afcon 2027 Barani Afrika kwa upande wa nchi wenyeji yaani Tanzania, Kenya na Uganda limezidi kushika kasi katika suala zima la maandalizi hususani miundombinu ambapo kwa sasa kila nchi imejikita katika maboresho na ujenzi wa viwanja vipya.

Thobias Masalu na Gilbert Ludovick
By Thobias Masalu na Gilbert Ludovick
19 Aug 2024
Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Tanzania inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Arusha, Uwanja mpya wa Dodoma lakini pia ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa, pamoja na ule wa Uhuru huku pia mpaka sasa tayari Kamati ya ndani ya Mashindano Afcon 2027 imezinduliwa.

Katika kuangazia mwendelezo wa Makala pamoja na habari za Afcon 2027, nimezungumza na Omary Katanga, Mwandishi wa Habari mzoefu na mchambuzi wa mpira nchini, ambaye kwa sasa anafanya kazi na Azam Media Ltd, amekuwa na uzoefu wa soka la Afrika ikiwemo kuandaa vipindi vya Michezo, kuchambua Mpira na kusafiri na vilabu mbalimbali kama vile Simba, Yanga, Azam na hata timu za Taifa za wanawake, wanaume na vijana zinaposhiriki katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo Klabu bingwa (CAFCL) na Kombe la Shirikisho (CAFCC).

Katanga ni miongoni mwa waliohudhuria katika Mashindano ya Afcon 2023 yaliyofanyika nchini Ivory Coast ambapo mwenyeji alitwaa ubingwa katika mchezo wa fainali dhidi ya Nigeria, mengi amejionea na kupata uzoefu na namna ambavyo mashindano hayo yaliandaliwa, katika Makala haya anaeleza uzoefu wake na nini Tanzania inaweza kujifunza. 

Omary Katanga akiwa Ivory Coast 

Karibu sana Omary Katanga, tunaangazia maandalizi ya Afcon 2027, ni miaka miwili kamili yaani 2025, 2026 tumebakiwa nayo kuelekea kufanyika kwa Afcon 2027 kwa mara ya kwanza katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, ulipokea vipi uamuzi wa CAF kuzipa nchi hizi uenyeji wa Afcon 2027?

Ahsante sana kwa kunialika, kwanza ni heshima kubwa sana kwa Tanzania kupata nafasi hii ya kuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa ushirikiano kati yake Kenya pamoja na Uganda, mchakato ulianza vizuri sana kwa serikali zote tatu na serikali yetu kwa maana ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye alikuwa kinara.

Mchakato ulipoanza tu wakapeleka zabuni ya pamoja na hatimaye kikao kwa wahusika wakaamua kwa maana ya Caf wenyewe kupitia Rais wake Dkt. Patrice Motsepe, akatangaza katika mkutano wao mkuu kwamba bid hii ama zabuni ya pamoja kwa Tanzania Kenya na Uganda, imefanikiwa kushinda na hivyo sasa tutakuwa wenyeji.

Wenyeji kwa maana kwamba kuna mechi ambazo zitapigwa Tanzania, kuna mechi zitapigwa Kenya na kuna mechi zitapigwa Uganda, vilevile Tanzania tutakuwa na viwanja viwili kwa maana ya miji miwili huku bara pamoja na kule visiwani Zanzibar kwenye uwanja wa New Amani Complex. 

Kwahiyo ni heshima kubwa sana kwa nchi hizi kujaribu jaribu kuomba wamefanya jambo la maana sana kwasababu wanasema usiwe muoga kuomba uenyeji wa mashindano fulani ilimradi tu ukishaona kuwa una uwezo wa kuwa mwenyeji basi ni kujaribu kuomba, kwasababu mataifa mengi sana yanayoomba, sasa kuthubutu kwa Kenya Uganda na Tanzania kwenda kuomba hatimaye imefanikiwa, na sasa tunajiandaa kwaajili ya kuwa wenyeji wa haya mashindano.

Haya ni Mashindano makubwa kabisa Afrika ambayo yanahusisha timu za Taifa,   na tumeshuhudia kabisa kwamba Tanzania imeweka historia ya kuwa katika haya mashindano mara tatu, utakumbuka mwaka 1980 tuliingia kwa mara ya kwanza katika mashindano haya ya Afcon, lakini vilevile mwaka 2019 halikadhalika tuliingia katika mashindano haya ya Afcon na mwaka 2024  mwezi January mashindano yalifanyika pale Ivory Coast tuliingia mara ya tatu. 

Timu ya Tanzania (Taifa Stars) katika Mashindano ya Afcon 2023 Ivory Coast

Maana yake kwamba tumeandika historia, na haikuwa rahisi hata kidogo kuingia kwenye haya mashindano kwa maana ushindani umekuwa mkali sana, lakini yote kwa yote ni kwamba upekee wa haya mashidano, ukubwa wa haya mashindano, unaifanya Tanzania kuandika historia yake ya pekee yake, kwa maana ya kwamba mwaka 2027 tunaingia kwenye historia nyingine, kwanza ya kuwa wenyeji lakini pia kushiriki mara ya nne ama ya tano kama tutafuzu kushiriki mwaka Afcon ijayo ya 2025 itakayofanyika Morocco.

Katanga umeshiriki Mashindano ya Afcon lakini pia Klabu Bingwa ukiwa mwandishi lakini pia ukiwa unauchambua mpira, nini Watanzania wafanye ili kuhakikisha kwamba maandalizi yanaenda na yanakuwa yanayofana mpaka kufikia 2027 kila kitu kiwe kwenye mstari wake?

Ukiachilia mbali maandalizi ya timu kwa maana ya timu za taifa, umezungumzia hapa nini watanzania wafanye unapozungumzia nini watanzania wafanye maanake unaelekeza moja kwa moja kwa upande wa mashabiki, Tanzania kuna vibe sana la mashabiki kuna mwamko mkubwa sana wa mashabiki.

Unakumbuka kila mwaka huwa tunafanya Matamasha ya Simba Day, Tamasha la siku ya Kilele Cha Mwananchi, ni matamasha ambayo yanavuta hisia na yanajaza umati mkubwa sana katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hii maanake ni kwamba mwamko wa soka kwa mashabiki wanaofuatilia mpira ni mkubwa, kwahiyo haya mashindano ya Afcon yanahitaji vibe ama mwamko wa aina hiyo ambao utaonesha alama kubwa tu katika upande wa Afrika na dunia kwa ujumla kuona kwamba Tanzania ina mwamko mkubwa sana wa mpira.

Simba Day 2024

Nikukumbushe historia moja, hivi karibuni tu timu ya Simba ilichaguliwa kushiriki mashindano ya African Football League (AFL) na Caf kwa mara ya kwanza ya mashindano hayo na yalizinduliwa hapa Tanzania, Simba ilicheza dhidi ya Al ahly ya Misri, utakumbuka Caf ndiyo walisema ufunguzi ufanyike hapa Tanzania. 

Umati mkubwa ulijitokeza, mwamko mkubwa ulioonekana hapa, uliionesha Caf kwamba Tanzania kuna mwamko wa kiasi gani kwa mashabiki, kwahiyo kitendo cha Caf kuiamini Tanzania katika ufunguzi wa hiyo michuano ya AFL ilileta hamasa kubwa sana na kusema kwamba kumbe Tanzania ni sehemu sahihi kabisa kwaajili ya kufanya matamasha makubwa kama haya kwa maana ya mashindano makubwa kama haya.

Sasa haya matamasha ya Simba, matamasha ya Yanga yana mwamko mkubwa sana, yana mchango mkubwa sana kuelekea 2027, kwasababu tunaipenda timu yetu ya Taifa, na hao mashabiki wa Simba  na Yanga na vilabu vingine wote wanaipenda timu yao ya Taifa na wala hakuna ubishi hata kidogo katika hilo.

Kilele cha Siku ya Wananchi (Yanga SC) 2024

 Na nina imani kabisa, kama watakuwa na mwamko huo huo wa matamasha waliokuwa nao, nina imani 2027 katika mashindano ya Afcon 2027, msisimko utaongezeka zaidi maanake tutaungana watanzania wote kwa pamoja kwahiyo itakuwa chachu kubwa sana.

Ilivyo bahati ni kwamba viongozi wetu wa vilabu Tanzania wamekuwa na kauli mbiu moja ambayo inahamasisha umoja, upendo lakini pia ule uungwana wa kiushangiliaji katika kuleta ile hamasa ya mchezo yenyewe kwahiyo wakichanganya vyote hivi tunategemea kuwa na mashindano mazuri, mashindano ambayo yanafana sana na mwamko utakuwa mkubwa kuliko ambavyo ilivyokuwa inatazamiwa hapo kabla.

Uganda Kenya nao wanajiandaa wanapoona Matamasha kama hayo unadhani kwamba watakaa kututazama maana tuna miaka miwili, 2025, 2026, kabla hatujaingia January 2027 ambapo Afcon itafanyika rasmi?

Inaweza ikawapa chachu kubwa na hili litakuwa jukumu lao Uganda na Kenya, angalia tu sasa hivi kwa msimu huu pekee yake wa mashindano timu zetu baadhi ambazo zinafanya matamashi haya zimealika timu kutoka nje ya nchi, Burundi imetoa timu tatu kuja kucheza katika matamasha haya, kule Mwanza timu ya Pamba imecheza dhidi ya  timu ya Vital’o ya Burundi, kule Kigoma Mashujaa FC imecheza dhidi ya Inter Stars kutoka Burundi, lakini Singida Black Stars wao pia wamecheza mechi yao dhidi ya Aigle Noir zote hizi zimetoka Burundi.

Kwahiyo unaona kabisa kwamba huu mwamko hizi timu zinaporudi, wataenda kusimulia kwamba ni kitu gani Tanzania wanafanya kwahiyo hii itawaambukiza, lakini Kenya pamoja na Uganda ambao timu zako hazijaalikwa kuja kucheza katika haya matamasha wanafahamu na wanafuatilia na inaweza ikawa ni hamasa kwao pia vilevile kuona kwamba kumbe na sisi tunaweza kuhamasishana, kama mashabiki, kama wana Kenya, kama wana Uganda kuwa na vibe ama mwamko kama ambao wanafanya Tanzania na ikatengeneza hamasa kubwa.

Sidhani kama Uganda na Kenya watakubali kufunikwa katika ombwe la mashabiki na Tanzania na wao pia kuna kitu watafanya na kama hawana mpango huo ni hamasa sasa tuwape wafanye huo utaratibu kufanya matamasha makubwa kama haya ambayo yanaweza kuleta mwamko mkubwa zaidi kama ambavyo yanavyofanyika hapa Tanzania  miaka iliyobaki siyo mingi kuelekea 2027, hawajachelewa bado wanaweza wakafanya hii ikaongeza hamasa zaidi  tukichanganya mataifa yote haya matatu Caf, Dunia, itajua kwamba kwanini nchi hizi tatu zimepewa kuwa wenyeji wa Afcon 2027.

Makala haya yataendelea Jumatatu ijayo

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Zipi 	Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?