Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili | The Dodoma Post
The Dodoma Post Makala

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanaendelea kushika kasi hasa kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha kila kitu cha lazima kwenye mashindano hayo kinakuwa tayari kwaajili ya kutumika ifikapo 2027.

thobias Masalu, Gilbert Lyimo
By thobias Masalu, Gilbert Lyimo
03 Sep 2024
Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alitembelea mradi wa ujenzi wa kiwanja kipya cha Dkt. Samia Suluhu Hassan August 29, 2024, kiwanja kinachoendelea kujengwa jijini Arusha.

Akiwa huko, Dkt. Ndumbaro aliwaomba wakandarasi wa mradi huo kufanya kazi kwa weledi na ufanisi huku akiwahakikishia kufika katika eneo hilo kwaajili ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi kila baada ya wiki mbili.

“Matarajio yetu ni kwamba mkandarasi atafanya kazi kwa wakati na atakabidhi mradi kwa wakati, tumeshamwambia mshauri mwelekezi ya kwamba amsimamie vizuri mkandarasi ili kazi iwe na ubora sana na amalize kwa wakati,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Ujenzi wa uwanja huo umefikia asilimia tano katika hatua ya awali ukihusisha uandaaji wa eneo la uwanja, manunuzi na ujenzi wa ofisi za mkandarasi.

“Uwanja huo ni maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishasema nataka Tanzania kwa kushirikiana na nchi wenyeji Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon 2027, maono yale ndiyo yamezaa mradi huu, tungekosa kuwa wenyeji sidhani kama mradi huu ungekuwepo leo,” ameongeza Dkt. Ndumbaro.

Waziri Dkt. Ndumbaro amewahakikisha wakazi wa Arusha kupata ajira za muda wakati wa ujenzi wa mradi huo, ikiwa ni sehemu ya kuwanufaisha wenyeji huku akiamini kuwa ujenzi utazingatia viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

“Kwa wana Arusha mradi huu ni muhimu sana kwenu, umekuja nyumbani kwenu tushirikiane na serikali katika kuhakikisha unakwenda vizuri, nimefanya maongezi na Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda naye ameniahidi atausimamia kwa karibu zaidi kwa sababu yeye yuko Arusha muda wote,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Uwanja huo unaojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 286 utakuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 30,000, vyumba vya watu mashuhuri, sehemu ya makumbusho na huduma nyingine ambazo zitaufanya utumike kila siku.

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Zipi 	Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?