LUKUVI AWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA DAWA ZA KULEVYA | The Dodoma Post
The Dodoma Post Kijamii

LUKUVI AWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA DAWA ZA KULEVYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu William M. Lukuvi amewasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2024, akibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia jitihada shirikishi za serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi.

Moreen Rojas
By Moreen Rojas
23 Jun 2025
LUKUVI AWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA DAWA ZA KULEVYA

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha taarifa hiyo,Waziri Lukuvi amesema dawa ya kulevya aina ya bangi imeendelea kuwa kinara kwa kukamatwa kwa kiasi kikubwa zaidi ambapo tani 2,307.37 zikiwa zimekamatwa mwaka 2024 pekee.

Amefafanua kuwa Kati ya hizo, tani 2,303.2 zilikuwa zimezalishwa ndani ya nchi, huku tani 4.17 zikiwa ni Skanka (bangi yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC) kutoka mataifa ya Kusini mwa Afrika na kwamba Skanka iliyokamatwa imeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka 2023, ikionyesha uimara wa udhibiti wa mipaka.

Kwa  upande wa dawa za kulevya zinazozalishwa viwandani, amesema Serikali ilikamata tani 1.7 za methamphetamine, kilo 433.02 za heroin na gramu 853 za cocaine.

"Kwa mara ya kwanza, dawa mpya aina ya methylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV) nayo ilikamatwa nchini ikiwa na uzito wa kilo tano,aidha, tani 18.45 za mirungi pia zilikamatwa kwenye operesheni mbalimbali, pamoja na kilo 56.78 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na tani 29.6 za kemikali bashirifu zilizokuwa zikijaribu kuingizwa nchini, "amesema.

Katika hatua ya kusaidia waathirika wa dawa hizo,Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutoa huduma ya tiba kwa waraibu kupitia vituo 16 vya methadone vilivyosajili waraibu 17,975, sambamba na nyumba 62 za upataji nafuu (sober houses) zilizohudumia waraibu 17,230 kwa mwaka 2024.

Waziri Lukuvi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kwa vitendo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ujumla.

Aidha, amewashukuru wataalamu wa afya, wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa pamoja na wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliosaidia kufanikisha hatua zilizofikiwa.

“Ushirikiano huu ni silaha muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya, kwani hili si tatizo la sekta moja linagusa afya, usalama, elimu, ajira, na ustawi wa jamii. Mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi jumuishi kutoka pande zote,” amesisitiza Lukuvi.

Aidha amewasihi wananchi kuendelea kuwa walinzi wa jamii kwa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi salama na huru dhidi ya athari za mihadarati.


Kwa upande wake  Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini Aretas Lyimo amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua wasanii wanaotumia kazi zao kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mavazi yanayochochea utumiaji wa dawa hizo, hasa kwa vijana.

Kauli hiyo imekuja kufuatia ongezeko la kazi za sanaa, hususan muziki na video, ambazo zimejaa maudhui yanayochochea matumizi ya mihadarati kwa njia ya picha, maneno na mitindo ya maisha inayooneshwa na wasanii hao.


Ameeleza kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa wakitumia majukwaa yao vibaya kwa kujihusisha na uvaaji wa nguo za aibu, pamoja na kuimba au kuigiza nyimbo zinazotukuza matumizi ya bangi na dawa nyingine haramu.

“Tunafuatilia kwa karibu nyimbo na video zinazochochea utumiaji wa dawa za kulevya, hatutasita kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria na maadili yetu,” amesema .

Amefafanua kuwa baadhi ya video za muziki zinazopatikana kwenye mitandao ya kijamii zimekuwa zikionesha wazi matumizi ya dawa hizo, huku mavazi ya wasanii wengi yakitajwa kuchochea mmomonyoko wa maadili kwa vijana wanaowachukulia kama mifano ya kuigwa.

Dkt.Tulia Aweka Jiwe La Msingi Ujenzi wa Shule ya Wavulana Bunge.

Dkt.Tulia Aweka Jiwe La Msingi Ujenzi wa Shule ya Wavulana Bunge.

Mavunde Akabidhi Jengo la kupumzikia Wananchi Hospitali ya Rufaa ya Dodoma

Mavunde Akabidhi Jengo la kupumzikia Wananchi Hospitali ya Rufaa ya Dodoma

Serikali kufanya mageuzi ya kimtazamo katika nafasi za uongozi kwa wanawake

Serikali kufanya mageuzi ya kimtazamo katika nafasi za uongozi kwa wanawake

Waziri Mhagama ametoa Agizo Vituo Vyote Vinavyotoa Huduma za Afya Viweke Wazi Mikataba Kwa Wateja

Waziri Mhagama ametoa Agizo Vituo Vyote Vinavyotoa Huduma za Afya Viweke Wazi Mikataba Kwa Wateja

CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA KUWA VINARA WA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME NA KUDUMISHA AMANI KWENYE MITAA YAO.

CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA KUWA VINARA WA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME NA KUDUMISHA AMANI KWENYE MITAA YAO.