

Benki ya Ushirika (Coop Bank) imeeleza kuwa inatumia Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (NaneNane) kama jukwaa muhimu kufikia wadau wake katika sekta ya ushirika, kilimo na mnyororo wa thamani wa kilimo-biashara, kwa lengo la kutoa elimu na huduma za kifedha.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 1, 2025 katika banda la benki hiyo kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Bw. Godfrey Ng’urah alisema benki hiyo ni mdau mkubwa katika kuendeleza sekta ya ushirika na kilimo nchini.
"Coop Bank imejikita katika kuwahudumia wanauchumi wa ushirika, wakulima na wananchi wote kupitia huduma za kifedha zinazolenga kuboresha mnyororo mzima wa thamani ya kilimo," alisema Bw. Ng'urah.
"Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu ili wapate elimu ya kifedha, kufahamu huduma mbalimbali tunazotoa, na kuelewa nafasi ya Coop Bank katika kukuza uchumi wa ushirika na kilimo nchini."
Aliongeza kuwa benki hiyo itakuwa inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi wote wanaotembelea maonesho hayo, ikiwemo ushauri wa kifedha, elimu ya huduma za kibenki, pamoja na fursa za mikopo kwa wakulima na vikundi vya ushirika.
"Tunashiriki pia kama wadhamini wakuu wa maonesho haya kwani Benki ya ushirika ni mdau namba moja wa Kilimo,soko letu mama katika masoko ya kisekta ni kilimo kwani wanaomiliki hisa zaidi ya asilimia 51% ya Benki yetu ni wakulima"Alisisitiza Bw.Ng'urah
Alibainisha kuwa mazao yote ya kimkakati kama vile kahawa, korosho, chai, ufuta, mbahazi na mengineyo yanapitia katika mifumo ya vyama vya ushirika (AMCOS na UNION), ambao ndio wateja wakuu na wamiliki wa benki hiyo. Coop Bank inatoa huduma za kifedha zinazolenga kusaidia ukusanyaji, usindikaji, masoko na uuzaji wa mazao hayo ndani na nje ya nchi.
“Tuna vyama vikuu vya ushirika kote nchini vinavyosimamia mifumo ya mauzo ya mazao ya wakulima. Hii ndiyo benki pekee inayomilikiwa na wanachama wa ushirika. Wakulima mmoja mmoja, AMCOS na UNION zote ni sehemu ya benki hii,” alieleza.
Bw. Ng’urah pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kuwa benki hiyo ilianza rasmi shughuli zake mwezi Oktoba mwaka jana na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili mwaka huu. Kwa sasa, Coop Bank ina matawi katika mikoa mitano: Kilimanjaro, Tabora, Moshi, Mtwara na Dodoma ambayo ni makao makuu.
“Tunawakaribisha wakulima, wafanyabiashara, vijana, wanawake na wadau wote wa kilimo kutembelea banda letu hapa katika eneo la wadhamini wakuu, na pia banda la Kijiji cha Ushirika. Katika mabanda haya mawili, tutakuwa tunatoa elimu, huduma na bidhaa zetu za kifedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo,” aliongeza.
Banda la Coop Bank linapatikana katika Kijiji cha Ushirika pamoja na eneo la wadhamini ndani ya viwanja vya maonesho ya Nzuguni, ambapo benki hiyo ni miongoni mwa wadhamini wakuu wa maonesho hayo yaliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Lengo la benki hiyo ni kukuza tija katika sekta ya uzalishaji kwenye kufikia malengo na maono mbalimbali kuelekea mpango wa mwaka 2050 unaotaka kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula duniani.
Benki hiyo ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan tarehe 28 Aprili 2025 katika ukumbi wa mikutano Jakaya Kikwete jijini hapa hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa Kitaifa na Kimataifa.
WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUHAMASISHA USHIRIKI WA WANANCHI KUPIGA KURA
WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE ZASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA KILIMO DODOMA.
MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MAONESHO YA NANENANE KITAIFA 2025.
TADB Yawawezesha Wakulima Wadogo Mikopo Yenye Dhamana Nafuu.
TUME YAVIHIMIZA VYOMBO VYA HABARI KURIPOTI HABARI ZA UCHAGUZI KWA USAHIHI
CCM Yatangaza Wagombea Nafasi Ya Ubunge Waliopenya Kwenye Mchujo:Mpina,Makamba Waenguliwa.
SHUJAA ALIYEPIGANA VITA ASISITIZA AMANI.
INEC YATANGAZA RASMI TAREHE YA UCHAGUZI MKUU 2025.
KATIBU BAWACHA AJIUNGA CHAUMA ATAJA SABABU YA KUONDOKA KWAKE.
VYAMA VYA SIASA VYAHAKIKISHIWA UWANJA SAWA UCHAGUZI MKUU 2025