DK.MPANGO AWATAKA WANANCHI KUTUMIA MIFUMO YA KIDIGITALI KUFANYA MALIPO,AIPONGEZA BoT KUZINDUA MFUMO MKUU JUMUISHI WA KIBENKI. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Tanzania

DK.MPANGO AWATAKA WANANCHI KUTUMIA MIFUMO YA KIDIGITALI KUFANYA MALIPO,AIPONGEZA BoT KUZINDUA MFUMO MKUU JUMUISHI WA KIBENKI.

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ametoa rai kwa wananchi kutumia mifumo ya kidigital kwa kufanya malipo ili kupunguza matumizi ya fedha mikononi lakini pia amewataka kuwa wazalendo kwa kutumia na kulinda mifumo iliyoanzishwa nchini

Sophia Kingimali
By Sophia Kingimali
30 Jul 2025
DK.MPANGO AWATAKA WANANCHI KUTUMIA MIFUMO YA KIDIGITALI KUFANYA MALIPO,AIPONGEZA BoT KUZINDUA MFUMO MKUU JUMUISHI WA KIBENKI.

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ametoa rai kwa wananchi kutumia mifumo ya kidigital kwa kufanya malipo ili kupunguza matumizi ya fedha mikononi lakini pia amewataka kuwa wazalendo kwa kutumia na kulinda mifumo iliyoanzishwa nchini

Pia amezitaka wizara na Taasisi za Serikali kuiga mfano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuwekeza katika Tehama na kutumia wataalamu wa ndani katika miradi mbalimbali ili kusaidia iweza kukamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Maagizo hayo ameyatoa leo Julai 30,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliotengenezwa na wataalamu wa BOT kwa kushirikiana na wataalamu wengine waliopo hapa nchini, ambapo kauli mbiu yake ikiwa "Tunaongoza mustakabali wa Teknolojia katika benki kuu za Afrika"lakini pia amezindua makumbusho ya kihistoria lakini pia maktaba ya kidigital 

amesema wizara na taasisi za serikali zinapaswa kuiga jambo hilo kwani litasaidia kukamilisha miradi kwa wakati.

Amesema kuwa kuundwa kwa mfumo wa iCBS kwa kutumia wataalamu wa ndani si tu mafanikio ya kiteknolojia bali udhibitisho wa uhuru uliyopo nchini.

“Hii ni tofauti na kipindi cha nyuma kilichopita ambapo watoa huduma wa nje waliweka mazingira ya utegemezi wa mifumo ya kidigitali kutoka kwao kwa maana ya ujuzi na vifaa tutoe kwao na wakati wa matengenezo tuwatafute, kwa kutengeneza mfumo huo imejidhihirisha kuwa nchi inaweza kujitegemea,” amesema Dk. Mpango

Amesema mfumo huo wa iCBS utaweza kudhibiti taarifa za kifedha jambo ambalo lina faida kubwa hasa katika dhama hizi za uhalifu wa kimtandao, changamoto za kisiasa za kimataifa huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwatumia wataalamu hao.

Hata hivyo Dk. Mpango ameitaka BOT kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakala wa Serikali Mtandao na wizara zinazohusika kuhakikisha zinausimamia vizuri mfumo huo na mingine yote ya malipo iliyopo ili nchi iendelee kupata matokeo stahiki ikiwemo kuimarisha uchumi wa nchi.

“Pia niwaombe mjikite kwenye matumizi sahihi ya mifumo wa kidigitali hasa katika kufanya miamala na malipo mbalimbali ili kupunguza matumzi ya fedha taslimu, BoT ongezeni kasi ya Taifa letu kuhamia kwenye malipo na uchumi wa kidigitali,” amesema

Sambamba na hayo Dk. Mpango akizungumzia kuhusu kukopesha pesa kwa njia ya mitandao amevionya vikundi vinavyokopesha fedha mitandaoni bila kutambulika kisheria wala kufuata utaratibu kwa kuwataka waache mara moja shughuli hizo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Aidha ameitaka BOT kuendelea kutoa elimu ya mikopo kwa wananchi lakini pia kuliangalia suala hilo na kuchukua hatua ili kuwahakikishia wananchi ambao wengi ni wakopaji wadogo hawaendelei tena kutapeliwa.

“Limeibuka wimbi la wakopeshaji fedha kupitia mitandao ya simu na kwamba licha ya kutotambulika kisheria wanaendesha shughuli hizo bila kufuata taratibu za ukopeshaji, wakopeshaji hao wanatoza liba kubwa, wanaingilia faragha za watu na hata kusambaza taarifa za wakopaji wao bila ridhaa, BOT shughulikieni jambo hili,” amesema

Aidha Dk. Mpango ameipongeza BOT kwa namna inavyoendelea kusimamia akiba ya fedha za kigeni ambayo kwa muda mrefu nchi haijawahi kushuka chini ya uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kinachopungua miezi minne. 

Kwa upande wake Naibu waziri wa fedha Hamad Chande amewapongeza wataalamu waliobuni mfumo huo huku akiwataka kuhakikisha mfumo huo wanaulind sana.

Akizungumza awali,Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa mfumo huo umetengenezwa na wataalamu wa benki hiyo kwa kushirikiana na wataalamu wengine waliopo nchini na kwa kutumia fedha za ndani.

“Wakati tunataka kutengeneza mfumo huu tulipata wazo wa kuutafuta sokoni, tulipoutafuta tulikuta unagharimu jumla ya Bilioni 91.9, lakini wataalamu hawa pamoja na kununua leseni, kuwaweka pamoja nje ya ofisi na gharama zao zingine jumla tumetumia Bilioni 10.6 hivyo tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. Bilioni 81,” amesema Tutuba

Amesema mifumo hiyo mikubwa ya kibenki kwa kawaida imekuwa ikitengenezwa na kampuni kubwa ya nje ya nchi lakini BoT imeweza kutimiza ndoto kwa kutumia wataalamu wao wa ndani na kwamba mfumo huo umekuwa na tija kwani umewasaidia kukabiliana na changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili hapo awali.

“Mfumo huu umeleta maboresho makubwa kwenye maeneo mengi ikiwemo utoaji wa taarifa sahihi za serikali, taarifa za miamala, ufungaji wa hesabu kwenye akaunti za wateja sasa zinafanyika kwa wakati, upatikanaji wa taarifa kwa wafadhili, ukokotoaji wa riba za kibenki na usimamizi wa ukwasi umeboreshwa,” amesema

Ameongeza kuwa uundwaji wa mfumo huo wa iCBS utawawezesha kupata taarifa papo kwa papo, kuondoa makosa ya kibinadamu, kuongeza usahihi wa taarifa, kuwapatia uwezo mkubwa wa maamuzi sahihi na kuongeza ujumuishi wa watu wengi zaidi kwenye huduma rasmi za fedha.

“Nawapongeza wataalamu wetu kwa ujasiri wao hasa wa kujitolea jambo ambalo limesaidia mfumo kukamilika kwa wakati, BoT tutaendelea kuusimamia vizuri mfumo huu na kuufanyia maboresho pale utakapotakiwa ili uweze kuwa imara na kufanyakazi kwa ufanisi,” amesema Tutuba

WAZIRI MKUYA AZIPONGEZA DIB, BoT KUSHUGHULIKIA UFILISI WA FBME

WAZIRI MKUYA AZIPONGEZA DIB, BoT KUSHUGHULIKIA UFILISI WA FBME

TBC KUAZIMISHA MIAKA 26 YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA HAYATI MWALIMU NYERERE KWA KUENDESHA MASHINDANO YA INSHA KWA WANAFUNZI.

TBC KUAZIMISHA MIAKA 26 YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA HAYATI MWALIMU NYERERE KWA KUENDESHA MASHINDANO YA INSHA KWA WANAFUNZI.

GAVANA TUTUBA: BENKI KUU ZIWE WASHIRIKA WA MAGEUZI YA KIUCHUMI

GAVANA TUTUBA: BENKI KUU ZIWE WASHIRIKA WA MAGEUZI YA KIUCHUMI

Rais Samia Azindua Dira Ya Taifa Ya Maendeleo 2050, Asisitiza Utekelezaji Wa Vitendo Na Upimaji Wa Matokeo

Rais Samia Azindua Dira Ya Taifa Ya Maendeleo 2050, Asisitiza Utekelezaji Wa Vitendo Na Upimaji Wa Matokeo