NFMC kushirikiana na Nesch Mintech kuanzisha maabara ya kisasa Saudi Arabia | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

NFMC kushirikiana na Nesch Mintech kuanzisha maabara ya kisasa Saudi Arabia

Kampuni ya New Future Mining Company (NFMC) imetangaza ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya Nesch Mintech Pvt Ltd ya Mwanza kuanzisha kituo kipya cha kisasa cha maabara ya uchunguzi na upimaji wa madini – NFMC LAB, kitakachojengwa jijini Jeddah, Saudi Arabia.

The Dododma Post
By The Dododma Post
26 Jun 2025
NFMC kushirikiana na Nesch Mintech kuanzisha maabara ya kisasa Saudi Arabia

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa NFMC, Mohammed Alomoudi, amesema kituo hicho kitaendeshwa na Nesch Mintech kwa kutumia utaalamu wenye viwango vya kimataifa vya ISO 17025:2017, na mbinu bora za kisasa kwa ajili ya kuhudumia kampuni za uchimbaji na utafiti wa madini katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

"Kwa kushirikiana na Nesch Mintech, tunapiga hatua muhimu katika kuleta maabara ya kiwango cha juu nchini Saudi Arabia. Ushirikiano huu unaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Saudi Arabia ya 2030 kwa kuhamasisha uwekezaji wa kiteknolojia, kuendeleza ujuzi wa ndani na kuhamisha maarifa kutoka kwa wataalamu wa kimataifa kwenda kwa mafundi wa Kisaudi," alisema Alomoudi.

Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gelead Teri, pamoja na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Ahmed Okeish.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nesch Mintech, Happiness Neganda Nesvinga, amesema kuwa NFMC LAB si tu itatoa huduma bora za maabara, bali pia itakuwa chachu ya maendeleo ya utaalamu wa ndani kupitia mafunzo ya kina kwa vijana wa Kisaudi.

"Tunalenga kuhakikisha kizazi kipya cha wataalamu wa madini kinakuwa tayari kukabiliana na ushindani wa kimataifa kupitia ubunifu na ubora wa huduma," alisema Nesvinga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gelead Teri aliipongeza Nesch Mintech kwa mafanikio hayo ya kuvuka mipaka na kuingia kwenye soko la kimataifa, akibainisha kuwa hatua hiyo inaonyesha uwezo mkubwa wa Watanzania katika kushindana kwenye tasnia ya sayansi na teknolojia duniani.

"Faida za ushirikiano huu ni pamoja na kuongezeka kwa ajira, uhamisho wa teknolojia, kukuza uchumi wa Tanzania na kuiweka nchi katika nafasi ya kuwa kitovu cha ubunifu na ubora wa sekta ya madini katika ukanda huu," alisema Teri.

Nesch Mintech, ambayo imekuwa ikihudumu nchini kwa zaidi ya miaka 10, ni kampuni ya kimataifa ya huduma za maabara ya madini, inayojulikana kwa ubunifu, usahihi wa kisayansi na mchango mkubwa katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na makampuni makubwa kuongeza thamani ya rasilimali zao.

Kupitia NFMC LAB, kampuni hiyo inaweka alama mpya ya ubora katika sekta ya madini duniani.

PPAA yatoa elimu matumizi ya Moduli Wiki ya Utumishi wa Umma

PPAA yatoa elimu matumizi ya Moduli Wiki ya Utumishi wa Umma

BRELA YAWEKA KAMBI KARIAKOO KUTOA HUDUMA YA KLINIKI YA BIASHARA KWA WAFANYABIASHARA

BRELA YAWEKA KAMBI KARIAKOO KUTOA HUDUMA YA KLINIKI YA BIASHARA KWA WAFANYABIASHARA

Sekta ya Madini Imechangia Katika Fedha Za Kigeni Hadi Kufikia Dola Bilioni 3.55

Sekta ya Madini Imechangia Katika Fedha Za Kigeni Hadi Kufikia Dola Bilioni 3.55

Sekta ya Uchukuzi Yachangia Dola za Marekani Bilioni 2.48

Sekta ya Uchukuzi Yachangia Dola za Marekani Bilioni 2.48

Mauzo Katika Soko la Jumuiya EAC Yameongezeka Hadi Kufikia Dola za Marekani Milioni 1,163.8

Mauzo Katika Soko la Jumuiya EAC Yameongezeka Hadi Kufikia Dola za Marekani Milioni 1,163.8