

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanachochea ukuaji wa utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na itikadi chanya ya utumishi kwa umma nchini.
Akizungumza jijini Dodoma baada ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali za serikali yanayoshiriki katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Waziri Simbachawene amesema kuwa taasisi nyingi zimepiga hatua kubwa katika kujenga mifumo ya kidijitali, hatua inayowezesha utoaji wa huduma kwa haraka, kwa ufanisi na kwa uwazi zaidi.
“Mabanda niliyotembelea yote yameonyesha maendeleo makubwa ya kidijitali. Mifumo hii inawasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi, jambo ambalo linakwenda sambamba na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha utoaji wa huduma kupitia TEHAMA,” amesema Simbachawene.
"Ni matumaini yangu kuwa mifumo hii ya TEHAMA itakayozinduliwa leo italeta mageuzi ya kiutendaji na kulifanya taifa letu kuendana na mapinduzi ya nne (4) ya Viwanda yanayotumia TEHAMA. Ni jambo la kihistoria sisi leo kuwa mashuhuda wa uzinduzi wa mifumo hiyo”
“Sasa ninaamini kila mmoja wetu anaweza kuwa shuhuda wa mageuzi katika utendaji kazi yanayotokana na uwepo wa mifumo iliyozinduliwa mwaka jana”
Mosi, mfumo e-Watumishi umeleta ufanisi katika uandaaji wa mishahara na watumishi wanapata kwa haki yao kwa wakati,
Pili, Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (e-Utendaji-PEPMIS) ambapo kila mtumishi wa umma anatakiwa kujaza utekelezaji wa shughuli anazofanya kila siku au kila wiki,
Tatu, Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) unatuwezesha kutambua mahitaji ya rasilimaliwatu katika utumishi wa umma na kuwafanya msawazo; na
Nne, Mfumo wa e-Mrejesho unasaidia watumishi na wananchi kwa jumla kuwasilisha maoni, mapendekezo, kero na maulizo kwa Serikali haraka.
Amezipongeza taasisi zote 185 zilizoshiriki kwenye maonesho hayo, akizihimiza taasisi ambazo bado hazijajiunga na mifumo ya kidijitali kufuata mkondo huo kwa haraka.
“Hongereni kwa taasisi zote 185 mlizoshiriki. Kwa zile ambazo bado, zifanye jitihada za kuunganishwa na mifumo hii kwa kuwa imeleta mageuzi makubwa katika utendaji kazi wa serikali,” ameongeza.
Aidha, Waziri Simbachawene amesisitiza kuwa taasisi zote za serikali zinapaswa kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa haraka na kwa gharama nafuu. Alitoa wito kwa wananchi kufika katika viwanja vya maonesho vilivyopo Dodoma kupata huduma mbalimbali moja kwa moja kutoka kwa taasisi za serikali.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Utumishi, Juma Nkomi amesema maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 15 hadi 23 Juni, ambapo kilele chake huadhimishwa rasmi Juni 23.
Amesema Tangu kuanza kwa wiki hiyo, taasisi mbalimbali za serikali pamoja na baadhi ya wizara zimekuwa zikitoa huduma moja kwa moja kwa wananchi na kuelezea shughuli zinazotekelezwa kwa mujibu wa majukumu yao.
“Maonesho haya yanatoa fursa kwa serikali kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi kuhusu huduma wanazopokea, pamoja na kero zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wakati,” amesema Nkomi
Maonesho hayo pia yameshirikisha baadhi ya sekretarieti za mikoa pamoja na halmashauri, hatua inayowezesha taasisi hizo kuwa karibu zaidi na wananchi wanaozihudumia.
Kwa mujibu wa waandaaji wa maonesho hayo, lengo kuu ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kutumia teknolojia na kushirikisha wananchi katika kujenga serikali bora.
Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni siku maalum ya Watumishi wa Umma ambayo husherehekewa tarehe 23 Juni kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Nchi zao na Bara la Afrika kwa jumla.
Chimbuko la Sherehe hizi ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers Nchini Morocco mwaka 1994. Uamuzi huo ulizitaka Nchi za Afrika kusherehekea siku hii kwa kaulimbiu moja katika Bara zima la Afrika.
Aidha, Mkutano wa nne wa Mawaziri wenye dhamana na Utumishi wa Umma uliofanyika Mwezi Mei 2003 uliamua kuwa Siku ya Utumishi wa Umma iwe ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Utawala Bora na Utumishi wa Umma chini ya Umoja wa Afrika (AU).
Kauli mbiu "Himiza Matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji"
KIHENZILE: UWAZI NA UWAJIBIKAJI NI NGUZO MUHIMU ZENYE TIJA KWA WANANCHI
KIHENZILE:WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NI FURSA MUHIMU KWA WANANCHI
ACT WAZALENDO KUUWASHA MOTO MANZESE WAJIDHATITI KUCHUKUA MAJIMBO YOTE DAR ES SALAAM
TANESCO YAJA NA KAMPENI MAALUM YA KUHAMASISHA ULIPAJI WA MADENI KWA WATEJA.
CDE SALUM ATANGAZA NIA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KAHAMA MJINI.
VIJANA WANAOTUMIA VIBAYA MITANDAO YA KIJAMII WAONYWA.
VIONGOZI WAANZA KUWAOGOPA WAJUMBE MOROGORO.
DODOMA YAELEKEA IRINGA KWA KISHINDO MASHINDANO YA UMISSETA.
Serikali Yatangaza Kuanza Msako Kuwabaini Wanaotumikisha Watoto
TANZANIA KUWA MWENYEJI TUZO ZA 32 ZA KIMATAIFA ZA UTALII.