Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2 | The Dodoma Post
The Dodoma Post Makala

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Jumatatu iliyopitia tuliishia kuangazia matamasha ya Simba Day na Wiki ya Kilele cha Wananchi, ambayo yamekuwa yakifanywa na Klabu kubwa nchini Simba na Yanga na namna ambavyo yamekuwa yakisisimua mpira wa miguu nchini na jinsi gani Kenya na Uganda wanaweza kutumia mwamko huo katika kuwasisimua mashabiki, wapenzi na wadau wa mpira katika mataifa yao, bado tuko naye Omary Katanga mwandishi na mchambuzi wa michezo mzoefu.

Thobias Masalu na Gilbert Lordivick
By Thobias Masalu na Gilbert Lordivick
27 Aug 2024
Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Katanga Ulikuwepo kwenye mashindano ya Afcon  yaliyomalizika February mwaka huu Ivory Coast na mwenyeji kutwaa ubingwa, kwa ulivyoona vitu gani unadhani Tanzania inaweza kujifunza kutokea kwenye mashindano hayo katika kuelekea maandalizi ya Afcon 2027?  

Cha kwanza kikubwa ni maandalizi, achilia mbali yale ya timu ya Taifa ambayo inashiriki kama timu mwenyeji, maandalizi ya nchi kwa ujumla wake, Serikali ya Ivory Coast wakati inaenda kuomba uenyeji wa haya mashindano ya Afcon walijipanga, walikaa wakatulia, wakaona kabisa kwamba kama sisi tunakuwa wenyeji, tufanye nini kuzidi wale walioandaa Mashindano yaliyopita, waliwaza juu ya maandalizi ya kinchi miundombinu ya viwanja, lakini pia hata huduma za usafiri, kwa wale mashabiki wanaokwenda uwanjani na kurudi kutoka viwanjani.

Simon Msuva Akishangilia baada ya Kufunga goli katika Michuano ya Afcon 2023 iliyofanyika Ivory Coast
Simon Msuva Akishangilia baada ya Kufunga goli katika Michuano ya Afcon 2023 iliyofanyika Ivory Coast

Moja kati ya kitu ambacho kilinishangaza na nilikipenda sana kama hata kwetu kitawezekana sina hakika ni suala zima la usafiri, unajua viwanja vingine viko mbali kidogo na mji, kwahiyo serikali ilikuwa imeandaa usafiri wa mabasi maalumu ambayo mashabiki hawalipi nauli, yanawatoa katikati ya miji yanawapeleka mashabiki katika maeneo ya viwanja ambavyo viko mbali na miji wanaangalia mechi mabasi yanawasubiri, baadae yanawapakiza na kuwarudisha katikati ya miji kila mmoja anaendelea na shughuli zake.

Kwahiyo hicho kitendo pekee yake kilileta hamasa za mashabiki kwenda uwanjani maanake mtu anafikiria kiingilio tu wala hafikirii suala la nauli maanake serikali tayari ishamaliza kila kitu.

Maandalizi yalikuwa ni mazuri, viwanja pia vilikuwa vizuri sana lakini vilevile ule uungwana, unajua unapoandaa mashindano makubwa kama haya unapokea watu kutoka mataifa tofauti tofauti ndani na nje ya Afrika ambao wanakuja na utamaduni tofauti kabisa.

Sasa wenye nchi yaani mwenyeji wa mashindano tabia zako zile za kiungwana ambazo unazozionesha pale, ni rahisi zaidi hawa wageni wanapokuja wakaiga, wakawa watulivu wakafuata mwenyeji anataka nini.

Lakini wewe mwenyeji wa mashindano ukawa na tabia siyo nzuri ambazo haziwezi kuigwa ni rahisi wale nao wakaja na tabia zao halafu ukajikuta sasa unachanganya vitu ambavyo vinaleta athari pia hata kwa watoto wadogo ambao wanakua wanakuja kushuhudia tabia zingine ambazo hazikubaliki.

Lakini ukitengeneza ustaraabu ukatengeneza uungwana kwa Taifa lako kama mwenyeji, wale wanaokuja wanaiga zile tabia na wanajizuia maanake unajua mpira wa miguu wakati mwingine una mihemko na wao sasa wanajikuta wanajizuia wanaenda mwenyeji anavyotaka mwenyeji anavyoelekeza inakuwa ni rahisi zaidi na wote mnakuwa mnafanana katika masuala ya tabia njema.

Inatajwa kwamba Watanzania siyo mashabiki wa mpira, bali wa Simba na Yanga, hili limekuwa likidhihirika hata kweye mechi za timu ya Taifa inapocheza, kumekuwa na changamoto ya mashabiki kwenda uwanjani, wakati mwingine serikali imekuwa ikilazimika kuondoa kiingilio ili kuwavutia mashabiki, lakini bado mechi huwa haijai, nini serikali ifanye kuelekea Afcon 2027 ili kuwasisimua baadhi ya mashabiki wanaomini katika Simba na Yanga pekee?

Kwanza kiingilio kidogo, waweke kiingilio kidogo huwa tunashuhudia mechi za timu za Taifa zote kwa mfano, hii ya wakubwa Taifa Stars, ya wanawake Twiga Stars, lakini kuna zile timu za vijana za Taifa za wanawake na wanaume kwa maana ya wasichana na wavulana, TFF kuna wakati hizi timu ukiachilia mbali na Taifa Stars hizi zingine Twiga Stars na zile za vijana kuna wakati zikicheza TFF hawaweki kiingilio kabisa malengo ni kufanya mashabiki wajae uwanjani kwaajili ya kwenda kushuhudia zile timu kuongeza ule ushangiliaji.

Ukiweka viingilio katika timu kama hizi, ni dhahiri umejiandaa kutokupata mashabiki kwasababu ni timu ambazo hazina mashabiki hata kama ni timu za Taifa, kwahiyo kitendo cha TFF kusema kwamba ingieni bila kuwa na kiingilio tunaona mashabiki huwa wanajaa wanafanya hivyo.

Sasa haya mashindano ya Afcon yanahusisha timu kubwa ta Taifa, tafsiri yake ni kwamba mataifa mengi yatakuja hapa, sijui utaratibu wa Caf inakuwaje katika masuala ya viingilio, lakini ingekuwa ni vizuri zaidi viingilio vikawa rafiki kwa watu mbalimbali kwaajili ya kuweza kuingia viwanjani, kitendo hiki pekee yake vitajaza viwanja.

Kwasababu mtu hatakuwa na mawazo tena, kwenda kuwaona sijui Taifa gani kuwaona Taifa fulani labda Ivory Coast, linakuja kucheza ukiwawekea kiingilio kidogo mashabiki huwa wanaitikia wanakuja na mashindano yatafana, kama inawezekana kuwa na jambo kama hilo la kupunguza kiingilio nadhani hicho ni kitu kikubwa cha kwanza.

Lakini jambo la pili ambalo serikali ya Tanzania inapaswa kufanya chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kabisa kwamba, kwanza wanakaa na wadau wote ambao wanaohusika na mchezo wa mpira wa miguu, kwa kuanzia na TFF wakae na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lakini pia wakae na baadhi ya viongozi katika Wizara inayohusika na masuala ya michezo waangalie ni kitu gani tufanye ili kuleta hamasa.

Lakini pia wasisahau kukaa na sisi wanahabari, sisi tuna mawazo, sisi ndo watu ambao huwa tunapiga kelele ya kutaka watu waende uwanjani, kwahiyo watuchague baadhi yetu tushirikishwe katika hivyo vikao tunaita mpango kazi, watuteue watushirikishe ili kutoa maoni yetu tuone jinsi gani ambavyo tutasaidia kujaza watu katika viwanja, hayo mambo mawili yakifanyika naamini kabisa kupitia hicho kikao tutaibuka na maazimio ambayo yatakuwa ni ya pamoja na watu watakuja uwanjani.

Katanga pale Ivory Coast ulitembelea viwanja vingapi ulipoenda kushuhudia Mashindano?
Viwanjani vingi kuna kiwanja kinaitwa Felix Houphouet-Boigny, uwanja wa Alassane Ouattara, viwanja hivyo nimehudhuria kwasababu mechi zilikuwa zinahama hama zinachezwa huku zinachezwa kule na nilifurahi sana.

Mambo gani ambayo uliyaona unaamini hata hapa kwetu yakifanyiwa kazi yataleta muonekano na madhari nzuri ya viwanja na kuvutia zaidi?

Cha kwanza kuondoa mabango uwanjani, yale mabango ambayo yanazunguka eneo la kuchezea sasa hivi teknolojia imekuwa kubwa, ukikaa jukwaani unaangalia mechi kwenye TV unaweza ukaona uwanja umeweka mabango kama mabango pembeni ya eneo la kuchezea lakini kumbe lile ni zulia (carpet) limechorwa lakini likipigwa na kamera linaonekana kama vile ni bango limesisima ni teknolojia hiyo wanaita 3D.

Sasa hiyo iondolewe sababu nafahamu mikiki mikiki hii na mabango yakikaa pembezoni mwa eneo la kuchezea kuna hatari sana kubwa kwa wachezaji kuumia, kwa sababu wachezaji wanatumia nguvu kubwa maana mara nyingi michezo kama hiyo huwa ni kama vita ya kulinda heshima ya Taifa husika, kwahiyo hiyo ikiwezekana basi yafanyike hayo kwasababu muda bado tunao tuna miaka zaidi ya miwili mbele, mabango yale kama ni lazima kukaa kwa maana ya biashara yatafutwe yale makapeti ambayo yamechorwa kwa mtindo wa 3D ili yakikaa pale tuone.

Mimi nilikuwa najiuliza kwamba sasa bango mbona linaonekana bango lakini mchezaji anakatiza pale anapita wala hajikwai lakini nilivyofika Ivory Coast kutembelea vile viwanja nikajiridhisha kwamba ile ni carpet ambayo imetandikwa ambayo imechorwa bango fulani kwahiyo ikipigwa picha na kamera ndiyo inaonekana kama bango lakini ni carpet ndiyo maana mtu anapita tu pale sasa hicho nadhani ni kitu kifanyike hasa katika eneo la kuchezea.

Lakini vilevile ukarabati mkubwa wa viwanja, najua uwanja wa Benjamin Mkapa unafanyika najua pia uwanja wa New Amani Complex Zanzibar umejengwa katika viwango vinavyokubalika, miundombinu yake imekaa imara kabisa sasa ni suala tu la kuhimiza sisi watanzania kwa maana ya bara na visiwani kulinda hii miundombinu isije ikaharibiwa.

Lakini kitu kingine cha kuongeza unajua tunaposafiri sisi katika mashindano makubwa kama haya huwa tunajifunza kulingana na kuona mambo ambayo yamewekwa pale hapa kwetu hivi viwanja vizingatie zaidi maeneo maalumu ya watu, maeneo ya waandishi wa habari yajulikane, maeneo ya viongozi, maeneo ya mashabiki mipaka ile ijulikane hawa wanaishia hapa wale wanaishia pale, hivi vitu vyote vikikaa katika mtindo ambao vimewekwa kitaalamu kwa kuona wenzetu wanavyofanya naamini kwamba yatakuwa mashindano ya kihistoria.

Umefika sehemu nyingi hapa Afrika hususani kupitia mchezo wa mpira wa miguu, suala la utalii na michezo hususani kwenye mashindano makubwa kama ya Afcon na Klabu bingwa likoje, na unadhani nchi inaweza kufanya nini kuhusianisha michezo na utalii katika Afcon 2027
Utalii unahusika moja kwa moja, Ivory Coast nilipokwenda kwaajili ya kutazama mashindano ya Afcon yaliyomalizika, ukipita tu barabarani kwanza wamening’ing’iza mabango yanayoizungumzia nchi yao, vivutio walivyonavyo, mambo yaliyomo katika nchi ya Ivory Coast, ukipita tu barabarani unaangalia juu wamening’ing’iza yale mabango yanayonesha wazi kabisa kwamba ukiwa Ivory Coast utaona hiki, utatembelea hapa, utakwenda hapa, huo ni utalii, wanaokwenda katika hiyo nchi lazima watatumia fedha kwaajili ya kupata huduma za kule michezo inahusianisha utalii moja kwa moja.

Morocco nilipokwenda kwenye mashindano ya Ligi ya mabingwa ya wanawake nilipokuwa na Klabu ya Simba Queens, halikadhalika ilikuwa hivyo hivyo hata katika siku za mechi uwanjani utaona kuna vitu mbalimbali vinawekwa mabango mbalimbali yanawekwa kuonesha kwamba hapa Morocco kuna moja, mbili, tatu ambapo mtu mwingine ukija unatamani kwenda kuona, ukipita barabarani unaona kuna vitu ambavyo vinaashiria kwamba upekee wa nchi yetu kuna hiki na hiki wewe mgeni ambaye unafika hapa utafaidika kwa kupata hiki na hiki na matokeo yake nchi itafaidika kwa kupata fedha za kigeni.

Ahsante Sana.

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Zipi 	Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?