

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita,Bohari ya Dawa (MSD) imeongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na MSD kutoka 7,095 mwaka 2021/2022 hadi 8,776 mwaka 2024/2025, idadi hii ni sawa na ongezeko la vituo 1,681.
Aidha, MSD imevihudumia vituo hivyo kupitia Kanda 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa leo Agosti 15, 2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD), Dodoma.
Aidha amesema kuwa Serikali ya Awamu Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kote nchini hatua iliyoongeza uwezo wa hospitali na vituo vya afya kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Katika kufanikisha jambo hili, Serikali imeitumia Bohari ya Dawa (MSD) katika Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya"Amesema
Katika kipindi cha miaka minne, Serikali kupitia Wizara Afya imetoa kiasi cha shilingi bilioni 642.1 kwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 196.3 kati ya bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 200 sawa na asilimia 98 ya fedha yote ya vituo kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya,Hii ni fedha nyingi kutolewa katika kipindi chochote tokea kuanzishwa kwa Bohari ya Dawa.
Aidha Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuongeza makusanyo ya fedha mwaka hadi mwaka kutokana na maboresho yanayoendelea yaliyowezesha kupatikana kwa bidhaa za afya kwa wingi katika maghala ya MSD zinazoendana na mahitaji ya vituo, kuongezeka kwa uwezo wa wateja kulipia bidhaa kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali na kuimarika kwa mahusiano kati ya MSD na wateja.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, makusanyo ya MSD yamekuwa makubwa kuliko kipindi chochote ambapo kiasi cha shilingi bilioni 184.2 kimekusanywa,Pia katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 30, 2025, Bohari ya Dawa imekusanya kiasi cha shilingi Bilioni 397.6.
“Kutokana na maboresho yanayoendelea na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya na mauzo ya bidhaa zilizosambazwa, mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/22, hadi kufikia shilingi bilioni 640 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 325 sawa na asilimia 103.1”
MSD imeendelea kuimarisha utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2025, hali ya utimizaji wa mahitaji ilikuwa asilimia 79 ikilinganishwa na asilimia 39 iliyorekodiwa mwaka wa fedha 2021/22. Ongezeko hili linatokana upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya na vituo kuendelea kuwezeshwa kufanya ununuzi wa bidhaa za afya.
Sanjari na hayo Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza thamani ya bidhaa za afya zinazonunuliwa kutoka kwa wazalishaji nchini. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, bidhaa za afya za thamani ya shilingi billioni 15.9 zilinunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani. Thamani hii imeendelea kuongezeka na kufikia shilingi billioni 98.72 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, Serikali inatambua umuhimu wa kusimamia na kukuza uzalishaji wa bidhaa za afya kutoka viwanda vilivyopo nchini ambapo Baadhi ya faida zinazopatikana kwa kufanikisha uzalishaji kutoka kwa viwanda vilivyo ndani ya nchi ni pamoja na kuhakikisha usalama wa masuala ya kiafya pale inapotokea dharura ya magonjwa au majanga mbalimbali, kutengeneza ajira, na kulinda akiba ya fedha za kigeni.
Kwa kipindi cha miaka minne, MSD imefanya ununuzi na usambazaji wa vifaa na vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini. Baadhi ya vifaa vilivyosambazwa ni pamoja na mashine za usingizi, CT- Scan, MRI 3T, Ultrasound mashine, na digital X-Ray vyenye jumla ya shilingi bilioni 429.2.
Serikali kupitia MSD imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za Mradi Msonge zinazohusu magonjwa maalum ya UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu na Ukoma zinaendelea kutolewa bure. Bohari ya Dawa imeendelea kutekeleza jukumu hili kwa kuhakikisha bidhaa hizi zinafika kwa walengwa. Katika kuimarisha utekelezaji endelevu wa Mradi Msonge, Bohari ya Dawa iliongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu kutoka asilimia 18 mwaka 2022 na kufikia asilimia 97 mwezi Desemba mwaka 2024 ambayo ilikuwa ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Global Fund mzunguko wa sita (GC6).
Aidha, katika kuhakikisha hakuna athari yoyote inayotokea kutokana na mabadiliko ya sera za nchi za nje za wadau wa maendeleo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili bidhaa zote zinazohusu magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ziweze kuendelea kupatikana nchini. Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeelekeza fedha zote zinazohitajika jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 142 kufanikisha ununuzi huo. Hatua hii inalenga kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizi kwa uhakika na wakati wote.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwasihi watanzania kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Amani Zanzibar ili kutoa hamasa Kwa wachezaji wa Taifa Stars sababu wamejitahidi na wanafanya vizuri kwani haijawahi kutokea kuongoza kundi kwa kuwa na pointi 9
“Watanzania napenda kuwaomba tujitokeze kujaza uwanja kwani Serikali imetumia pesa nyingi kwaajili ya kuandaa mashindano haya”
WATANZANIA WAASWA KUJITAFAKARI KABLA YA KUCHUKUA MIKOPO.
TUKITUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA TUTAOKOA HEKTA 400,000 ZA MISITU ZINAZOTEKETEA KWA MWAKA-MJIOLOJIA NSAJIGWA.
MHANDISI SANGA AONGEZA MWEZI MMOJA KLINIKI YA ARDHI KIVULE KUONGEZA KASI YA UTOAJI HATI
SERIKALI YAFUNGUA MILANGO YA FURSA, KWA WAKULIMA WA MWANI TANGA
WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA KATIKA UTEKELEZAJI WA MAUDHUKUMU YAO HASA KATIKA KIPINDI HIKI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025
Serikali Inaendelea Kuimarisha Mazingira Kuwawezesha Vijana Kuanzisha Shughuli Za Uzalishaji Mali.
NGO's zatakiwa Kuwa Mawakala wa mabadiliko chanya katika Jamii.
INEC YAMKABIDHI FOMU ZA UTEUZI MGOMBEA URAIS WA CHAMA CHA NLD DOYO HASSAN DOYO
MGOMBEA KITI CHA URAIS KWA TIKETI YA CHAMA CHA NRA ACHUKUA FOMU TUME
TUME YA TEHAMA NA TAASISI YA KASI KUJA MWAROBAINI WA UDUKUZI MTANDAONI.