Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi | The Dodoma Post
The Dodoma Post Makala

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Waandaji wa Afcon 2027 Tanzania Kenya na Uganda wako kwenye maandalizi yenye kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanyika kwa ustadi na ubora ili kujenga imani kwa miaka mingine pia kupata fursa kama hiyo.

Thobias Masalu Gilbert Lordivick
By Thobias Masalu Gilbert Lordivick
10 Aug 2024
Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

July 5, 2024 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua Kamati ya Kitaifa ya Ndani ya Wadau ya Maandalizi ya AFCON 2027 (LOC), huku ikikabidhiwa majukumu ya kuhakikisha maandalizi yote yanafanyika kwa ufasaha na kwa ufanisi ili kukidhi matakwa yote yanayotakiwa na Shirikisho la Mpira Barani Afrika (CAF) pamoja na lile la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Kamati hiyo inayoundwa na wadau wa masuala mbalimbali ikiwemo michezo, uchumi, ulinzi na usalama, sera imekabidhiwa majukumu ya kuhakikisha maandalizi yote ya ndani yanayohusiana na Mashindano hayo yanafanyika kwa wakati na pia kuishauri serikali katika mambo yote yanayohusiana na maandalizi ya kuelekea Afcon 2027.

“Tumeunda kamati yenye weledi ndani ya nchi, na tunatarajia kupata ushauri unaotupeleka kwenye mafanikio makubwa kwahiyo msisitize kutushauri chochote mnachoona kinaweza kutusaidia.”

Waziri Mkuu alisema kamati hiyo itahusika katika kuhakikisha kwamba taarifa, maarifa, ujuzi na uzoefu walionao wana kamati unapaswa kutumiwa vyema na serikali ili kukamilisha maandalizi kwa weledi na ustadi kwaajili ya kuleta mageuzi ya michezo nchini pamoja na kunufaika na kuwepo kwa mashindano katika sekta mbalimbali.

“Kamati hii tumeteua na sekta binafsi tukijua kwamba mashindano haya yatagusa kila sehemu, serikali itawajibika, sekta binafsi ina nafasi yake, Miundombinu, hili halina shida, mpango ulishawekwa na kazi inaendelea na kamati mnao uhuru wa kuomba kwenda kuona popote maandalizi ya miundombinu yetu ambayo sisi sasa hivi tunaitaka tuitumie, uzoefu wenu wa kuona na kushiriki Mashindano mbalimbali ya nje ya nchi tunataka muulete hapa na mtushauri serikali kwahiyo mnao uhuru wa kufanya hivyo kila mmoja kwa nafasi yake awe tayari kutoa ujuzi wake.”

Kamati hiyo pia imekabidhiwa majukumu ya kuhakikisha inashiriki vyema katika kuiandaa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ili isiwe timu shiriki bali timu shindani katika mashindano hayo kama ilivyokuwa kwa Ivory Coast katika mashindano yaliyotamatika February mwaka huu.

“Tunayo Timu ya Taifa na timu yetu ya taifa miaka mingi imekuwa ikicheza michezo nje ya nchi, na mwenendo wa timu yetu tunapocheza nje mnaujua lazima tufanye mabadiliko ya haraka ili na sisi tuwe kama Senegal, uwezekano wa wenyeji kuwa washindi ni mkubwa na inawezekana haitapendeza sana sisi tuwe wenyeji halafu baadae tugeuke tuwe washangiliaji, lazima tuingie kwenye maandalizi thabiti ya timu ya taifa, wadau mnasemaje wachezaji wakongwe mnasemaje, nini tufanye tupate timu ya taifa ambayo itakwenda kuibuka kuwa mshindi wa Afcon 2027, hilo ni jukumu lenu.”

Kamati hiyo ambayo ni miongoni mwa kamati kuu nyingine tatu zilizoundwa kwaajili ya maandalizi ya Mashindano ya Afcon 2027 ikiwemo pia, Kamati kuu ya Kitaifa ya Maandalizi Afcon 2027 (Executive Committee) pamoja na ile Kamati ya Kitaifa ya Ufundi ya Maandalizi ya Afcon 2027 (Technical Committee) inayo nafasi ya kusukuma mbele agenda zote za maandalizi na kushiriki kutoa mawazo yenye weledi yatayosaidia kufanyika kwa Afcon ya mfano barani Afrika.

“Uwepo wenu katika kamati hii ni imani ya serikali kwenu wadau kwamba mna uwezo wa kusimamia jambo hili tunawafahamu tumeona kazi zenu, tumeshuhudia matunda ya kazi zenu, tumeona mnaweza kusimamia maandalizi haya ya Afcon kwa pamoja na serikali tukapata mafanikio makubwa.”

Kuzinduliwa kwa kamati hiyo inaashiria kuwa, inapaswa kila mmoja kwa nafasi yake kutambua kuwa Afcon 2027 inafanyika nchini hivyo inayo fursa ya kuitangaza Tanzania na maandalizi yake kila sehemu na kwa kila mdau ambaye anaweza kushiriki katika maandalizi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza, “Afcon Afcon Afcon, nchi ijue, Jumuiya ya Afrika Mashariki ijue, Bara la Afrika lijue na dunia ijue kwamba Afcon 2027 inafanyika huko, nataka niwaambie Afcon inafanyika kwenye nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda wapi itachezwa itategemea na maandalizi ya ndani, miundombinu, utulivu wa kisiasa, ulinzi na amani ndani ya nchi, sisi tutaendelea kujiimarisha tunataka tuwe na viwanja vingi ndani ya nchi, michezo mingi ichezwe ndani ya nchi, wawe na uhakika wa huduma, wawe na uhakika na utulivu wa kisiasa ndani ya nchi, wawe na uhakika wa usalama.” 

Kamati imesisitizwa kuhakikisha kwamba inakuwa tayari kubeba majukumu hayo ambayo serikali inaamini kuwa kwa uzoefu, wa wajumbe pamoja na viongozi wa kamati hiyo watayabeba na kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika maandalizi ya mashindano makubwa ya kimichezo. 

“Jukumu hili naomba mlipokee na sisi ndiyo tunajua nyinyi ndiyo wabebaji wa jukumu hili zito lakini ni muhimu kwenu kulibeba ili tuweze kufika kwa pamoja, ubunifu wenu mawazo yenu, mnaweza mkatengeneza mfumo mzuri tu wa kwenda kuhakikisha kwamba tunapata Timu ya Taifa nzuri ambayo itakwenda moja kwa moja kwenda kupata kombe na sina mashaka katika hili.”

Kamati hiyo inaundwa na watu mbalimbali akiwemo, Leodgar Tenga Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ayoub Mohammed Mahamoud Makamu Mwenyekiti, Neema Msitha Katibu wa Kamati, Said Kassim Marine Katibu Msaidizi, huku wajumbe wake wakiwa ni Wallace Karia, Dr. Suleiman Mahamoud Jabir, Nehemia Mchechu, Wilfred Kidao, Ally Mayay, Ameir Mohamed Makame, Najima Said Shaame, Mohamed Abdulaziz, Prof. Madundo Mtambo, Jacquline Kawishe, Geliad Teri, Aboubakar Bakhresa, Prof. Mohamed Janabi, Abubakar Liongo, Kanali Mstaafu Thomas Ndonde, Rhona Lymo, Dr. Ramadhan Dau, Brigedia General Hassan Mabena, Abdulmajid Nsekela, SSP Jumanne Muliro, Abdul Mhinte, Salleh Ally, Hamad Abdallah, Johson Palangyo na Kheri Salum Ally.

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Zipi 	Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?