KAGERA, GEITA WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA UBORESHAJI | The Dodoma Post
The Dodoma Post Siasa

KAGERA, GEITA WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA UBORESHAJI

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kagera na Geita kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
25 Jul 2024
KAGERA, GEITA WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA UBORESHAJI

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kagera na Geita kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 25 hadi 26 Julai,2024 Mkoani Kagera.

Mafunzo kama hayo pia yamefunguliwa Mkoani Geita na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele leo mkoani humo.

“Kwa kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” amesema Jaji Mbarouk.

Amesema kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu na amewataka kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.

 

Aidha, Jaji Mbarouk amesema matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” amesema Jaji Mbarouk.

Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya Bukoba, Frola Alex Kaijage

Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.

“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mbarouk

Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.

Katika hatua nyingine, Jaji Mbarouk amewaambia watendaji hao kuwa wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

Jaji Mbarouk ametoa angalizo kwa mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma Julai 20, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).

Uzinduzi huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2024, na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”

MONGELLA ATARAJIA KUFANYA ZIARA SHINYANGA.

MONGELLA ATARAJIA KUFANYA ZIARA SHINYANGA.

NMB BUNGE BONANZA KUSAIDIA UJENZI WA SHULE YA WAVULANA BUNGE.

NMB BUNGE BONANZA KUSAIDIA UJENZI WA SHULE YA WAVULANA BUNGE.

JUKWAA LA MWAKA LA MASHIRIKA YASIYO YAKISERIKALI KUFANYIKA DODOMA.

JUKWAA LA MWAKA LA MASHIRIKA YASIYO YAKISERIKALI KUFANYIKA DODOMA.

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO AMEAGIZA  KUHARAKISHWA KWA SHERIA YA ADHABU  ILI IPELEKWE BUNGENI KUFANYIWA MAAMUZI.

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO AMEAGIZA KUHARAKISHWA KWA SHERIA YA ADHABU ILI IPELEKWE BUNGENI KUFANYIWA MAAMUZI.

BVR KITS 4,257 KUBORESHA DAFTARI SHINYANGA NA MWANZA.

BVR KITS 4,257 KUBORESHA DAFTARI SHINYANGA NA MWANZA.