BRELA YAWATAKA WASANIFU MAJENGO NA WAJASIRIAMALI KUTUMIA VIZURI BUNIFU ZAO. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

BRELA YAWATAKA WASANIFU MAJENGO NA WAJASIRIAMALI KUTUMIA VIZURI BUNIFU ZAO.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa rai kwa wasanifu Majengo kutumia vizuri bunifu na kulinda michoro yao lakini pia wajasiriamali nao wakitakiwa kuongeza ubunifu katika vifungashio na mikebe ili kuzipa thamani bidhaa zao jambo litakalosaidia kuhimili ushindani kitaifa na kimataifa.

Sophia kingimali
By Sophia kingimali
05 Sep 2024
BRELA YAWATAKA WASANIFU MAJENGO NA WAJASIRIAMALI KUTUMIA VIZURI BUNIFU ZAO.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa rai kwa wasanifu  Majengo kutumia vizuri bunifu na kulinda michoro yao lakini pia wajasiriamali nao wakitakiwa kuongeza ubunifu katika vifungashio na mikebe ili kuzipa thamani bidhaa zao jambo litakalosaidia kuhimili ushindani kitaifa na kimataifa. 

Hayo yamebainishwa leo, Septemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa  BRELA Godfrey Nyaisa, katika kikao kazi kilichowakutanisha  na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili na kupata maoni ya Rasimu ya Mkataba wa Sheria ya kimataifa inayohusu Ulinzi wa Maumbo Bunifu na Michoro.

Nyaisa, amefafanua kuwa maoni hayo watayawasilishwa kwenye mkutano wa Kideplomasia wa nchi Wananchama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) ambapo Tanzania ni mwanachama utakaofanyika, Riyadh nchini Saudi Arabia kuanzia Nov. 11 hadi 22 mwaka huu.

“Mkataba wa WIPO wa Sheria ya Maumbo Bunifu unalenga kuweka utaratibu au mfumo wa Kimataifa wa Usajili na Ulinzi wa Maumbo Bunifu kwa nchi na Mashirika Wanachama, mfumo huu utawezesha uwasilishaji wa maombi ya ulinzi wa maumbo bunifu kupitia WIPO ambapo mwombaji ataweza kuwasilisha ombi moja na kuchagua nchi zaidi ya moja zitakazokuwa zimeridhia mkataba huo ambazo anahitaji kupata ulinzi wa ubunifu wake,” amesema.

Amesema kuwa mfumo huo utaongeza wigo wa ulinzi katika nchi  nyingi kwa mara moja badala ya nchi moja kwa moja ambazo mbunifu anahitaji kulinda ubunifu husika jambo linalosaidia kupunguza gharama na ugumu wa ulinzi wa bunifu hivyo kikao hicho ni muhimu kwa wadau kutoa maoni.

Ameweka wazi kuwa endapo sheria hiyo itapitishwa na Tanzania kuridhia ni dhahiri itatoa fursa na kuongeza wigo kwa wabunifu wa maumbo, michoro bunifu wa Kitanzania kusajili na kulinda kazi zao katika ngazi ya kimataifa na kukuza biashara zao jambo litakalosaidia kuweza kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.

Amesisitiza kwamba kulingana na ushindani uliopo kibiashara kwa sasa kitaifa na kimataifa kinachotakiwa kwa watanzania kuiongeza ubora wa bidhaa, huduma na muonekano unaovutia kuanzia kwenye bidhaa husika, vifungashio, mikebe kwa lengo la kuongeza thamani na iwe rahisi kutambulika na kuvuta wanunuzi.

Pia amefafanua kwamba ili kuhakikisha watanzania wanafanya vizuri BRELA, imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali na wabunifu ili waweze kufanya bunifu zitakazowawezesha kutambulika kirahisi sokoni na kuhimili ushindani.

“Ili kuhakikisha elimu ya masuala ya Miliki Bunifu inawafikia wadau wengi tumejipanga kutashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Miliki Kanda ya Afrika (ARIPO) kutoa mafunzo kwa wakufunzi, Novemba mwaka huu kwa lengo la kupata idadi kubwa ya wakufunzi ambao watatoa elimu kwa wajasiriamali lukuki hapa nchini na kuhakikisha, Miliki Bunifu inakuwa chachu ya maendeleo ya kukuza uchumi kama ambayo nchi zilizoendelea zinafanya,” amesema.

Kwa upande wake Mustafa Haji, ambaye katika kikao hicho alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji  wa BPRA, Khamis Juma Khamis, ametoa rai kuwa vikao kama hivyo ni vema pia kikafanyika Zanzibar kwa lengo la kuendelea kushirikiana kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

Naye, Mhadhiri wa UDSM, Dk Perfect Melkiori, amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imejitokeza kwa wanafunzi katika chuo hicho ni wengi wa wanafunzi na wafanyakazi, kutojua thamani ya bunifu zao jambo linalofanya kurubiniwa na baadhi ya kampuni na mashirika ili kuuza bunifu zao kwa bei ndogo.

Dk Melkiori ambaye pia ni Meneja wa Miliki Bunifu wa chuo hicho, amesema kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi na wafanyakazi, kwa sasa wanaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kundi hilo halipotezi haki ya kwa kuuza bunifu kwa gaharama ndogo kutokana na kurubuniwa na kampuni na mashirika.

TRA yaahidi kuwa na usawa kwa wafanyabiashara Nchini

TRA yaahidi kuwa na usawa kwa wafanyabiashara Nchini

VIONGOZI SOKO LA MACHINGA DODOMA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI

VIONGOZI SOKO LA MACHINGA DODOMA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI

MCHENGERWA AZINDUA MFUMO WA KADI JANJA ZA MWENDOKASI AWATAKA DART NA UDART KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA MAGARI.

MCHENGERWA AZINDUA MFUMO WA KADI JANJA ZA MWENDOKASI AWATAKA DART NA UDART KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA MAGARI.

MRAJISI VYAMA VYA USHIRIKA AGUSWA NA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO YA TTCL.

MRAJISI VYAMA VYA USHIRIKA AGUSWA NA HUDUMA YA MALIPO KWA MKUPUO YA TTCL.

MWENYEKITI WA BODI YA T-PESA AWATAKA WANANCHI KUWA WAZALENDO.

MWENYEKITI WA BODI YA T-PESA AWATAKA WANANCHI KUWA WAZALENDO.