Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa amesema SERIKALI imekuja na mwarobaini wa kudhibiti upotevu wa mapato katika mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa kuzindua mfumo wa kisasa wa kukusanya nauli kutumia kadi janja huku akitoa rai DART kwa kushirikiana na. UDART kuhakikisha inatatua changamoto ya uhaba wa mabasi yaendayo haraka kabla ya Desemba mwaka huu kwa kuwakaribisha Watanzania kushiriki katika zabuni kwa Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Septemba 2,2024 katika uzinduzi wa kadi janja na mageti katika mfumo wa DART, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa amesema mfumo huo utasaidia kuzuia udanganyifu na kuongeza mapato ya serikali huku akiagiza kadi hizo zianze kutumika mara moja.
Amesema uzinduzi huo unatokana na maendeleo ya teknolojia ya ukusanyaji wa nauli kwa DART, ambayo inaufanya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kuwa katika kiwango cha juu kabisa.
“Niwapongeze DART kwa kutibu hoja za wananchi, uzinduzi wa kadi janja na kuachana na matumizi ya karatasi unaleta mapinduzi makubwa ya namna tunavyotaka kuwahudumia Watanzania katika usafiri wa Dar es Salaam, inakwenda kujibu hoja na kutatua changamoto za wananchi za kulipa nauli,
“ Ninatambua hapo awali wananchi walipata changamoto nyingi , ukisoma katika mitandao ya kijamii, kila Mtanzania analalamika, wapo waliokuwa wanalalamika kuhusu nauli zao, wapo waliokuwa wakitoa fedha zikiwa nyingi kupata chenji inachukua muda mrefu na wakati mwingine kukosa, sasa mfumo huu utajibu maswali yao ya muda mrefu,” amesema.
Aidha ameagiza upatikanaji wa kadi hizo kuwa rahisi bila changamoto na DART kuongeza ufanisi kila anayetumia mwendo kasi afurahie kuishi Dar es Salaam, huku serikali ikijipanga kwenda katika majiji mengine pindi changamoto zote zikitatuliwa.
Mchengerwa amemtaka Mtendaji wa DART na UDART kutekeleza suala la muda wa mabasi kukaa kituoni na kuwa wakali kwa watumishi wasiosikia kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwahudumia Watanzania.
Amesema hatamani na hafurahishwi kuona watu wakikaa kituoni muda mrefu na wakati mwingine mabasi yakiwapita bila kuwachukua hivyo ameagiza changamoto hiyo itatuliwe haraka.
“Ni kweli kuna changamoto ya mabasi, Watanzania wanasubiri mabasi kwa njia ya Kimara uhitaji ni mabasi 170 na Mbagala ni 500, DART hakikisheni mabasi yanapatikana kabla ya Desemba, mwaka huu na muwakaribishe Watanzania kushiriki zabuni kwa Dar es Salaam, waje kushirikiana na serikali katika uwekezaji,” amesema.
Aidha Mchengerwa amewataka watendaji hao zinapotokea changamoto zitatuliwe mara moja kwani hataki kuona mabishano katika masuala ya biashara, wasikae ofisini watoke kuwabaini wasiofanya kazi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Athuman Kihamia amesema mfumo wa kukusanya nauli wa kisasa wa kutumia kadi janja utasaidia kuepuka kutumia mfumo wa karatasi au keshi hali itakayopelekea utunzaji wa mazingira.
“Mfumo huu uliojengwa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka unafaida nyingi ikiwa kuondoa matumizi ya karatasi yanayochangia uchafuzi wa mazingira.
“Pili kuondokana na suala la usumbufu katika chenji kwani ukizingatia nauli sehemu nyingi ni sh.750, hiyo sh.50 imekuwa ikileta usumbufu na muda mwingine haipatikani, pia hupunguza muda wa kupanga foleni kulipa nauli katika vituo vyetu,” ameeleza.
Amesema kadi hizo zina ubora tofauti na zinazotumia maeneo mengine kwani zina vitu vingi ambavyo mtu anaweza kutumia sio kulipa tu nauli.
DKT. BITEKO ataka TANESCO kuongeza kasi utekelezaji miradi ya umeme wa gridi
Ndaisaba azidi kumwaga Fedha katika sekta ya Michezo Wilayani Ngara
"Hatutawavumilia wanaochochea Machafuko Nchini" Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan
(LHRC) chatoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama Kufuatia mauaji ya watoto watatu wa familia moja
TRA yaahidi kuwa na usawa kwa wafanyabiashara Nchini
VIJANA NDIO WALINZI WA NCHI HII: MEJA JENERALI RAJABU MABELE
BRIGEDIA Jenerali Ngata Apongezwa uongozi makini SUMAJKT
VIONGOZI SOKO LA MACHINGA DODOMA WASIMAMISHWA KUPISHA UCHUNGUZI
TRA yaahidi kuwa na usawa kwa wafanyabiashara Nchini
(LHRC) chatoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama Kufuatia mauaji ya watoto watatu wa familia moja