LIPUMBA: WAKATI WA MABADILIKO NI SASA, CHAGUENI CUF KUJENGA NCHI YA HAKI SAWA KWA WOTE | The Dodoma Post
The Dodoma Post Siasa

LIPUMBA: WAKATI WA MABADILIKO NI SASA, CHAGUENI CUF KUJENGA NCHI YA HAKI SAWA KWA WOTE

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema wananchi wana kila sababu ya kudai haki na kuleta mabadiliko kupitia chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele kutetea usawa kwa wote.

Sophia Kingimali
By Sophia Kingimali
12 Oct 2025
LIPUMBA: WAKATI WA MABADILIKO NI SASA, CHAGUENI CUF KUJENGA NCHI YA HAKI SAWA KWA WOTE

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema wananchi wana kila sababu ya kudai haki na kuleta mabadiliko kupitia chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele kutetea usawa kwa wote.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Kiburugwa, Jijini Dar es salaam Profesa Lipumba amesema mwaka huu Watanzania wana bahati kubwa kwa kuwa CUF imesimamisha wagombea wa nafasi zote kuu — urais, ubunge na udiwani — ambao ni “watu wa watu” wazalengo na wana uchungu wa kweli kwa wananchi.

“Umaskini unaoendelea nchini ni matokeo ya sera mbovu za chama tawala, CCM. Tuliahidiwa vita dhidi ya maadui watatu — ujinga, maradhi na umaskini — lakini hadi sasa hawajaonyesha wamefikia wapi. Badala yake wanaendelea kutuambia watafanya nini kwa siku 100,” alisema Prof. Lipumba.

Aliongeza kuwa Tanzania imebarikiwa ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana endapo serikali itakuwa na sera makini za kilimo na viwanda. “Ni wakati wa kuwachagua viongozi watakaotumia fursa tulizonazo kujenga uchumi imara na kupunguza umasikini,” amesisitiza.

Aidha Prof. Lipumba amesema vyanzo vya kodi katika halmashauri ni vingi, lakini kutokana na ubadhirifu na miundombinu mibovu, huduma za afya, maji na elimu zimeendelea kuwa duni. Alitoa wito kwa wananchi wa Kiburugwa na maeneo mengine ya Dar es Salaam kuchagua viongozi waadilifu watakaowezesha maendeleo ya kweli.

Aidha, aligusia rasilimali za madini hasa dhahabu, akisema Tanzania ni nchi ya tatu kwa mauzo ya dhahabu barani Afrika, lakini wananchi hawafaidiki kutokana na “mikataba ya kitapeli.”

“Tukiwa na serikali isiyo na rushwa tunaweza kutumia madini haya kuanzisha viwanda na kutoa ajira kwa vijana. Tunahitaji wabunge waadilifu, wenye moyo wa nchi, si wabinafsi,” alisema.

Prof. Lipumba alieleza kuwa serikali ya CUF itahakikisha wazee wanapata kipato cha msingi, huku ikiwekeza zaidi katika elimu, afya na teknolojia ili Watanzania waweze kufanya kazi popote duniani.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Prof. Lipumba ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CUF, akisema hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta haki na mabadiliko ya kweli.

Prof. Lipumba pia amewataka Jeshi la Polisi kuhakikisha haki inasimamiwa wakati wa kampeni na uchaguzi, huku akionya dhidi ya vitendo vya kuchana mabango ya wagombea.

 “Usitumie umaskini wa watu kuwapa pesa wachane mabango. Huko juu CCM wakanyeni watu wenu. Hatutaki vurugu, tunataka amani na hoja,” amesisitiza.

Amewataka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha mawakala wanakuwepo vituoni kabla ya kuanza kwa uchaguzi na kumtaka Naibu Katibu wa Tume, Kailima, kuhakikisha watendaji wote wanazingatia taratibu.

Aidha ametoa wito wake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Prof. Lipumba amesema: “Mama Samia, weka lengo. Ikiwa mgombea mwingine atashinda, ukubali matokeo na uheshimu maamuzi ya wananchi.”

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CUF Jimbo la Mbagala, Said Kinyogoli, amesema anagombea kwa moyo wa uzalendo na dhamira ya kuwatumikia wananchi.

 “Nikiingia bungeni nitajenga hoja, nitapongeza na nitakosoa. Ninakwenda kuwafuta machozi watu wa Mbagala,” alisema Kinyogoli.

Ameahidi kushughulikia changamoto za wakina mama wanaoteseka kwa mikopo, kuhakikisha fedha zinawafikia kwa wakati, na kusimamia upatikanaji wa ajira kwa vijana.

WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29

WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29

Kihongosi: Kampeni za CCM Zimejikita Katika Maadili,Utu na Mshikamano wa Kitaifa.

Kihongosi: Kampeni za CCM Zimejikita Katika Maadili,Utu na Mshikamano wa Kitaifa.

KUPIGA KURA NI HESHIMA, WAJIBU NA SILAHA YA KIDEMOKRASIA

KUPIGA KURA NI HESHIMA, WAJIBU NA SILAHA YA KIDEMOKRASIA

RAI AHAIDI KUTOA GARI LA KUBEBEA MAITI KILA KATA JIMBO LA TEMEKE.

RAI AHAIDI KUTOA GARI LA KUBEBEA MAITI KILA KATA JIMBO LA TEMEKE.

MWAGO AHAIDI KUTUMIA ASILIMIA 10 YA MSHAHARA WAKE KULETA MAENDELEO JIMBO LA MBAGALA

MWAGO AHAIDI KUTUMIA ASILIMIA 10 YA MSHAHARA WAKE KULETA MAENDELEO JIMBO LA MBAGALA