Nala Dodoma Kuwa Kitovu cha Viwanda, Wawekezaji Wajitokeza | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

Nala Dodoma Kuwa Kitovu cha Viwanda, Wawekezaji Wajitokeza

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), imeendelea kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika maeneo maalum ya kiuchumi yaliyotengwa na Serikali ambapo katika eneo la Nala, jumla ya wawekezaji wazawa wanne wameonesha utayari wa kuwekeza

Moreen Rojas, Dodoma
By Moreen Rojas, Dodoma
23 Sep 2025
Nala Dodoma Kuwa Kitovu cha Viwanda, Wawekezaji Wajitokeza

Hayo yameelezwa leo Septemba 23, 2025 na Meneja wa Kanda ya Kati wa Mamlaka hiyo, Venance Mashiba mbele ya Wandishi wa Habari waliotembelea eneo la uwekezaji la Nala lililopo jijini Dodoma ikiwa ni programu iliyoandaliwa na TISEZA kwa ajili ya kutoa elimu kwa Waandishi hao ili wapate uelewa wa maeneo hayo na kuendelea kuhamasisha uwekezaji kupitia vyombo vya habari.

Meneja Mashiba amesema kuwa, wamewapeleka Waandishi wa Habari katika eneo hilo ili wajionee eneo lilivyo na mazingira yaliyowekwa na serikali kwa ajili ya kuvutia uwekezaji.

"Tunaendelea kuhamasisha wawekezaji wengi kuwekeza hapa Nala kwani maeneo haya yana huduma zote muhimu, mpaka sasa tuna kiwanda kimoja ambacho ujenzi wake unakaribia kukamilika na wawekezaji wanne wazawa wameleta maombi ya kupatiwa maeneo. Pia, tunaendelea na mazungumzo na wawekezaji wa nje. Tunatoa rai kwenu Waandishi wa Habari kutusaidia kuhamasisha kupitia vyombo vya habari ", amesema Meneja Mashiba.

Amewaeleza Waandishi hao sifa ambazo zimetolewa na Mamlaka hiyo kwa wawekezaji wanaohitaji nafasi hiyo kuwa ni uwekezaji uwe na thamani isiyopungua Dola za Marekani milioni 5 kwa muwekezaji wa ndani na uwekezaji usiopungua thamani ya Dola za Marekani milioni 10 kwa muwekezaji kutoka nje, uwekezaji kuweza kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 100 pamoja na kuwa na teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Pendo Gondwe amesema kuwa eneo hilo lina jumla ya hekta 607 ambalo litakuwa na viwanda mbalimbali vikiwemo vya dawa, usindikaji wa mazao, utengenezaji wa magari na miradi ya teknolojia na viwanda vingine ambapo matarajio ya serikali ni kulifanya eneo hilo kuwa na viwanda vingi ifikapo mwaka 2030.

"Tunahakikisha tunatangaza fursa kwa Watanzania watakaohitaji kuwekeza, tunatarajia itakapofika Disemba angalau viwanda 100 viwepo kwenye maeneo maalum ya kiuchumi ikiwemo Nala", amesema Pendo.

Amesisitiza kuwa, Serikali imetoa ardhi bure ili kuhamasisha uwekezaji wa haraka ambapo muwekezaji atatakiwa kujenga kiwanda ndani ya mwaka mmoja. Ametaja vivutio vingine vya uwekezaji katika maeneo maalum kuwa ni pamoja na kuondolewa kodi kwenye baadhi ya maeneo na kupunguziwa kodi kwenye uingizaji wa mitambo na malighafi.

FCC  YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

FCC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

DC Nyamwese aanika fursa za uwekezaji Handeni

DC Nyamwese aanika fursa za uwekezaji Handeni

CRDB WATOA GARI LA PILI KWA MSHINDI,WATANZANIA WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA.

CRDB WATOA GARI LA PILI KWA MSHINDI,WATANZANIA WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA.

Kodi Sasa Si Kikwazo: Wafanyabiashara Wazidi Kuunga Mkono Serikali.

Kodi Sasa Si Kikwazo: Wafanyabiashara Wazidi Kuunga Mkono Serikali.

BRELA YAFANYA KAZI NZURI YA URASIMISHAJI BIASHARA MWANZA

BRELA YAFANYA KAZI NZURI YA URASIMISHAJI BIASHARA MWANZA