TANESCO YAZINDUA KAMPENI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Nishati

TANESCO YAZINDUA KAMPENI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imezindua rasmi programu ya Konekt Umeme, Pika kwa Umeme inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania.

Sophia Kingimali
By Sophia Kingimali
09 Oct 2025
TANESCO YAZINDUA KAMPENI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imezindua rasmi programu ya Konekt Umeme, Pika kwa Umeme inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Oktoba 9, 2025, katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke, na mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chalamila amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu matumizi ya nishati safi na salama kwa afya na mazingira.

 “Huu ni mwanzo wa zama mpya katika utekelezaji wa sera ya nishati safi nchini. Programu hii inaimarisha jitihada za Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya umeme wa uhakika na kuacha matumizi ya nishati zinazochafua mazingira,” alisema Chalamila.

Ameongeza kuwa matumizi ya umeme kwa kupikia ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, hatua inayolenga kuhifadhi misitu na kuboresha afya za wananchi hasa wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alisema programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Energy Compact—mpango wa kitaifa wa nishati uliozinduliwa na Wizara ya Nishati—unaolenga kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu kwa wananchi wote.

“Kupitia mpango huu, TANESCO inalenga kuunganisha wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, huku programu ya Konekt Umeme, Pika kwa Umeme ikitoa majiko ya umeme kwa gharama nafuu kwa wateja wapya, wakilipia kidogo kidogo kupitia mfumo wa token,” alieleza Twange.

Amesema hatua hiyo inaendana na malengo ya Sera ya Nishati ya mwaka 2015 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambazo zote zinatambua nishati safi kama nyenzo ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

Mratibu wa programu hiyo amesema Konekt Umeme, Pika kwa Umeme inalenga si tu kuongeza matumizi ya nishati safi, bali pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kupikia kwa umeme ikiwemo ufanisi, usalama na gharama nafuu kwa muda mrefu.

Mwisho wa hafla hiyo, Mhe. Chalamila aligawa majiko ya umeme kwa wananchi mbalimbali na kuwataka kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi katika jamii zao.

“Tunataka kuona wananchi wanabadilika kifikra na kivitendo. Kutumia umeme kupikia si anasa tena, bali ni utekelezaji wa sera ya maendeleo endelevu,” amesisitiza.

TANESCO YATEKELEZA KWA MAFANIKIO PROGRAMU YA “KONEKT UMEME, PIKA KWA UMEME” NCHI NZIMA

TANESCO YATEKELEZA KWA MAFANIKIO PROGRAMU YA “KONEKT UMEME, PIKA KWA UMEME” NCHI NZIMA

TANESCO YAPATA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA KWA WATEJA 2025.

TANESCO YAPATA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA KWA WATEJA 2025.

RC CHALAMILA AZINDUA PROGRAMU YA KONEKT UMEME,  PIKA KWA UMEME

RC CHALAMILA AZINDUA PROGRAMU YA KONEKT UMEME, PIKA KWA UMEME

TANESCO YAKUTANA NA WADAU MOROGORO KUJADILI MIKAKATI YA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI BWAWA LA JNHPP

TANESCO YAKUTANA NA WADAU MOROGORO KUJADILI MIKAKATI YA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI BWAWA LA JNHPP

UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE WAIMARIKA

UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE WAIMARIKA