Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu | The Dodoma Post
The Dodoma Post Kijamii

Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania kulinda amani ya nchi, hasa taifa linapoelekea katika Uchaguzi Mkuu, wakisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
22 Oct 2025
Viongozi wa dini Kaskazini wahimiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wamewataka Watanzania kulinda amani ya nchi, hasa taifa linapoelekea katika Uchaguzi Mkuu, wakisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa.

Viongozi hao kutoka mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro wametoa kauli hiyo leo Oktoba 22, 2025 katika Kongamano la Amani na Uchaguzi lililofanyika mjini Moshi.

Mwishoni mwa kongamano hilo lililoongozwa na kauli mbiu 'Kupiga kura ni haki yetu na amani ya nchi yetu ni wajibu wetu', viongozi wa Dini wamesoma maazimio, yanayosisitiza ulinzi wa amani ya nchi na kuhimiza wananchi kushiriki katika uchahuzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akisoma maazimio hayo, Katibu wa  BAKWATA Wilaya ya Moshi, Alhaji Awadhi Lema ametaja mambo saba yaliyokubaliwa na viongozi wa dini kuwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi waliojiandikisha kuhakiki majina yao na kujitokeza kupiga kura.

Azimio jingine ni kuwataka Watanzania kuepuka uchochezi kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, Vyombo vya dola kutumia hekima na busara kulinda amani siku ya uchaguzi, kupanua ushiriki wa viongozi wa dini katika vyombo vya maamuzi na utungaji wa sheria pamoja na kila mwananchi kuwa na wajibu wa kulinda amani wakati wa kudai haki yake.


 

Akizungumza katika Kongamano hilo, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mlewa Shaban, amesema hakuna amani ya kweli bila haki, usalama wa uhai na mali. 

Amefafanua kuwa, jukumu la kulinda amani si la serikali pekee bali ni la kila raia, akisisitiza umuhimu wa kuepuka chuki, uongo na maneno ya kuchochea mgawanyiko.

“Kuua mtu mmoja ni sawa na kuondoa amani kwa jamii nzima na raia mwema ni yule anayejenga amani kwa wengine. Amani hujengwa kwa uvumilivu, uadilifu na kuheshimiana bila kujali tofauti za kidini, kikabila au kisiasa,” amesema Sheikh Mlewa.

Mwanasheria wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mch. Wakili Daniel Swai aliyemwakilisha Askofu Fredrick Shoo, amesema amani na haki haviwezi kutenganishwa, kwani vinashikamana katika kujenga jamii yenye heshima na mshikamano.


Naye Padri Steven Msami kutoka Kanisa la Anglikana Tanga amesema amani ni tunda takatifu, na palipo na amani watu hukaa kwa utulivu. 

“Tusiseme amani tu, bali tuseme na uvumilivu, kwani bila uvumilivu hakuna amani,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Elinawinga Mariki amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha na kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi wenye hekima na busara.

Katibu wa Bakwata, Mkoa wa Arusha, Ally Athuman Nassoro, amesisitiza kuwa amani haina mbadala, hivyo Watanzania wanapaswa kuilinda kila wakati wanapokutana na changamoto.

“Tumuombe Mungu atupe uongozi utakaoleta maisha bora kwa Watanzania,” amesema.

Yakoba Hassan,  ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kinamama Waislamu Moshi, aliomba vyombo vya ulinzi na usalama kuepuka kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa uchaguzi, ili kudumisha amani iliyopo.

Awali akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava, amesema Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi wa kikatiba na kidemokrasia huku hali ya amani ikiendelea kutawala mkoani humo.

“Tunaendelea kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kwa sababu ni haki yao ya msingi. Serikali itahakikisha usalama na haki vinatawala katika mchakato mzima wa uchaguzi,” alisema Mzava.

Aliongeza kuwa serikali inafarijika kuona viongozi wa dini wanashirikiana katika kulinda amani, kwani maoni na ushauri wao ni mchango muhimu kwa serikali na jamii.

 

AMANI NDIYO HIFADHI YA MWANADAMU, TUILINDE- VIONGOZI WA DINI

AMANI NDIYO HIFADHI YA MWANADAMU, TUILINDE- VIONGOZI WA DINI

WAHADZABE WA KARATU WAISUBIRI KWA HAMU OKTOBA 29

WAHADZABE WA KARATU WAISUBIRI KWA HAMU OKTOBA 29

89 WAKAMATWA KUJIHUSISHA NA DAWA ZA KULEVYA.

89 WAKAMATWA KUJIHUSISHA NA DAWA ZA KULEVYA.

NECTA:WATAKAOJIHUSISHA NA UDANGANYIFU MTIHANI WA DARASA LA NNE KUCHUKULIWA HATUA.

NECTA:WATAKAOJIHUSISHA NA UDANGANYIFU MTIHANI WA DARASA LA NNE KUCHUKULIWA HATUA.

RC MAKALLA AZINDUA MSIMU WA SHEREHE ZA MILA ZA KIMASAI

RC MAKALLA AZINDUA MSIMU WA SHEREHE ZA MILA ZA KIMASAI