HISTORIA YAANDIKWA RAIS DK.SAMIA APOKEA SH.TRILIONI 1 KAMA GAWIO NA MICHANGO MINGINE. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Tanzania

HISTORIA YAANDIKWA RAIS DK.SAMIA APOKEA SH.TRILIONI 1 KAMA GAWIO NA MICHANGO MINGINE.

Rais wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Leo, Juni 10, 2025 amepokea kiasi cha Sh1.028 trilioni kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamimizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
10 Jun 2025
HISTORIA YAANDIKWA RAIS DK.SAMIA APOKEA SH.TRILIONI 1 KAMA GAWIO NA MICHANGO MINGINE.

Rais wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Leo, Juni 10, 2025 amepokea kiasi cha Sh1.028 trilioni kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamimizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.

Makusanyo hayo ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina mwaka 1959, ni ongezeko la asilimia 68 ya kiasi kilichokabidhiwa mwaka jana kipindi kama hiki na asilimia 34 ya makusanyo yote ya mwaka 2023/24, ambayo yalikuwa ni Sh767 bilioni.

Kuna uwezekano wa takwimu hizo kupaa zaidi kwani makusanyo bado yanaendelea mpaka Juni 30 mwaka huu, ongezeko linaloshuhudiwa ni  matokeo ya mwitikio chanya wa taasisi za umma  katika kutekeleza maelekezo ya . Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuongeza tija na ufanisi

Rais Samia alionesha kuridhishwa na mwenendo huu ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo yake kwa taasisi kuongeza tija na ufanisi katika utendaji hivyo asema kuwa anajivunia uwekezaji wa Sh86.3 trilioni uliofanywa na serikali kwenye taasisi za umma na kampuni zinazomilikiwa kwa sehemu na Serikali.

Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amesema kiwango hiko bado hakijafikia matarajio ya Serikali juu ya mchango wa Mashirika na Taasisi za Umma katika mfuko mkuu wa Serikali wa mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa Taasisi za Umma.

“Lengo letu ni kufikia angalau Shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka ujao, na nina imani tunaweza, Nikutake, Msajili wa Hazina (Nehemiah Mchechu), kuzipitia taasisi zote na kuweka malengo mahsusi ya mapato kwa kila moja, ili tuweze kufikia azma hiyo."Amesema.

Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa mashirika na hatimaye ukusanyaji mapato yasiyo ya kikodi na utoaji gawio mwakani, Mhe. Rais ameagiza mambo manne ikiwemo Taasisi kuwa wabunifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji na kutatua changamoto zinazowakabili.

“Mageuzi ni pamoja na kuwa wabunifu, tusisubiri Serikali itatue kila changamoto inayotukabili kama taasisi. Tutumie fursa mbalimbali zinazotuzunguka katika kutatua changamoto hizo ikiwemo soko la mitaji,” amesema  Rais Dk Samia.

Sanjari na hilo,  amemwagiza Waziri wa Mipango na Uwekezaji prof.Kitila Mkumbo kuendelee kusimamia ukamilishaji wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma kwani usimamizi madhubuti wa uwekezaji wa Serikali, tunapaswa kuhakikisha kuwa kunakuwa na Sheria ya Uwekezaji wa Umma ikiwemo suala la Mfuko,
 

Sambamba na hilo, Mhe. Rais alimuagiza Msajili wa Hazina pamoja na vingozi wote wa Taasisi za Umma kuendelea kubuni na kusanifu mifumo ya TEHAMA kwani mifumo ya TEHAMA mahsusi itaongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao na hatimae kusaidia utoaji huduma wa haraka na kuongeza faida kutokana na uwekezaji uliopo.

“Ninataka muendelee kuhuisha mifumo ya TEHAMA iliyopo ili iweze kuwa na mlingano mzuri wa taarifa na kuongeza tija kwa taasisi zetu,” amesisitiza.

aidha Rais ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mamlaka nyingine husika kuendelea na jitihada za jumla za kuwajengea watumishi uwezo katika nyanja mbalimbali za kisasa pamoja na motisha stahiki.

Akizungumza awali, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema kiasi cha Sh1.028 trilioni kimekusanywa kutoka katika jumla ya taasisi na Mashirika 213 (195 ya umma na 18 Kampuni zenye hisa chache).Hii inamaanisha kuwa Mashirika 57 hayajatoa gawio bado--- ambayo ni asilimia 22 ya Mashirika yote.

“Tutaendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Mchechu.

Kwa upande wake Waziri Prof. Kitila Mkumbo ameahidi kuendelea kuhakisha wizara yake inasimamia kikamilifu maono ya Rais ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kutoa matokeo bora kwa maendeleo ya Taifa.

Katika mwaka ujao wa fedha 2025/26, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imejipanga kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha usimamizi na tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.

“Lengo letu ni kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi hizi zinaendelea kutoa matokeo bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” amesema Prof. Kitila.

Katika tukio hilo la kihistoria ‘ Gawio Day’, Rais Samia ametoa tuzo kwa taasisi 14 zilizofanya vizuri zaidi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Washindi walichaguliwa kwa kuzingatia vigezo vya mchango mkubwa kwa Serikali, uendelevu wa michango, ukuaji wa michango, na mageuzi ya kiutendaji.

Katika kundi la taasisi zilizotoa gawio kubwa zaidi, Twiga Minerals Corporation iliongoza kwa kutoa Sh93.6 bilion, ikifuatiwa na Airtel Tanzania kwa Sh73.9 bilioni, na NMB Bank Plc kwa Sh68.2 bilioni.

Katika kundi la taasisi zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iliongoza kwa Sh181.1 bilioni, ikifuatiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)----Sh38.8 bilioni na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)----Sh29.8 bilioni.

Kwa taasisi zilizoongeza michango yao kwa kasi zaidi, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ziliongoza.
TPDC iliongeza gawio lake kwa asilimia 100, NHC kwa asilimia 363 na Benki ya Kilimo kwa asilimia 285.

Katika kundi la taasisi zilizotoa mchango mfululizo kwa miaka mitano, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zilitambuliwa kwa uendelevu na nidhamu ya kifedha.

BRELA yatoa Gawio la Shilingi Bilioni 20.4 kwa Serikali

BRELA yatoa Gawio la Shilingi Bilioni 20.4 kwa Serikali

TUME YA UCHAGUZI YAPONGEZWA MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU 2025

TUME YA UCHAGUZI YAPONGEZWA MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU 2025

Rais Samia kupokea gawio la kihistoria, wachumi watarajia makubwa

Rais Samia kupokea gawio la kihistoria, wachumi watarajia makubwa

VITONGOJI 284 ARUMERU MASHARIKI VYAFIKIWA NA UMEME

VITONGOJI 284 ARUMERU MASHARIKI VYAFIKIWA NA UMEME

RAIS SAMIA Ni Mkombozi wa Maendeleo katika Nchi yetu:Mmuya

RAIS SAMIA Ni Mkombozi wa Maendeleo katika Nchi yetu:Mmuya