Asali ya Tanzania Yapata Kibali Kuuzwa China. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Tanzania

Asali ya Tanzania Yapata Kibali Kuuzwa China.

Katika hatua kubwa inayotarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya ufugaji nyuki, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kusaini makubaliano na Serikali ya China, kuruhusu uuzaji wa asali ya Tanzania kwenye soko la China.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
15 Aug 2024
Asali ya Tanzania Yapata Kibali Kuuzwa China.

.Makubaliano haya yanafuatia jitihada za muda mrefu za kuhakikisha bidhaa za asali kutoka Tanzania zinapata nafasi ya kuuzwa katika soko kubwa zaidi duniani.

Akizungumza leo Agosti 15,2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uwekaji saini itifaki ya kuuza asali ya Tanzania nchini China, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula, alieleza kuwa kufunguliwa kwa soko la China ni matokeo ya mawasiliano ya muda mrefu kati ya nchi hizi mbili, ambayo yalianza mwaka 2018.
"Huu ni ushindi mkubwa kwa wafanyabiashara wa asali nchini. Sasa wanaweza kuuza bidhaa zao kwenye soko lenye mahitaji makubwa zaidi duniani," alisema Mhe. Kitandula.

Kitandula pia alibainisha kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo, wafanyabiashara wa asali watatakiwa kuhakikisha kuwa wanakidhi vigezo vya kimataifa vya usalama wa chakula na afya, ikiwa ni pamoja na kusajili makampuni yao kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na Usalama wa Vyakula, Afya ya Mimiea na Ulinzi wa Mazingira.

Amesema ili kufanikisha hilo, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeanzisha dawati maalum la kusaidia wafanyabiashara hao kujisajili kwa njia ya kidigitali. Hata hivyo amesema hadi sasa ni kampuni 12 tu ndizo zimejisajili kwenye mfumo huo, hivyo ametoa rai kwa kampuni ambayo bado hazijasajiliwa kujisajiliwa.

Pamoja na hayo amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha rasilimali zilizopo, ikiwemo misitu, nyuki na wanyamapori zinaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.

"Jitihada zake za uhifadhi wa rasilimali hizi, Rais Dk. Samia ameendelea kutangaza na kuvutia wawekezaji katika sekta yetu ya ufugaji nyuki. Uongozi wake umekuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Maliasili na Utalii, huku akilenga sio tu kutunza mazingira na bionuwai, bali pia kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali.

“Ufugaji nyuki ni sekta muhimu ya kiuchumi inayoathiri moja kwa moja maisha ya wananchi, hasa wale wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Sekta hii imekuwa chanzo cha ajira kwa takribani watu milioni mbili, hususan vijana na wanawake, na inachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania.

“Tanzania ina maeneo makubwa ya misitu yenye ukubwa wa hekta milioni 48.1, ambayo inawezesha uzalishaji mkubwa wa asali. Ingawa nchi ina uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali kwa mwaka, kwa sasa inazalisha tani 33,276, sawa na asilimia 24.1 ya uwezo huo. Pamoja na changamoto hizo, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali Afrika Mashariki na SADC, na nafasi ya pili barani Afrika, ikionesha umuhimu wa sekta hii kwa uchumi wa taifa,” anasema Mhe. Kitandula.

"Ufugaji nyuki ni moja ya shughuli ya kiuchumi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida hususan wale wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Shughuli hiyo imekuwa ni chanzo muhimu cha ajira, hasa kwa vijana na wanawake, ambapo takribani watu milioni mbili nchini wamejiajiri kupitia ufugaji nyuki,"amesema.

Anaongeza kuwa, ingawa Tanzania inazalisha kiwango kikubwa cha asali, ni asilimia tano tu ya asali hiyo inayouzwa nje ya nchi, kutokana na masharti mbalimbali ya kibiashara. Asali na nta ya Tanzania huuzwa hasa katika masoko ya Ulaya, Marekani, na Mashariki ya Kati, na mauzo haya huipatia nchi wastani wa dola milioni 12.9 za Kimarekani kila mwaka, sawa na shilingi bilioni 30.58.

Kitandula amesisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji na ubora wa asali, huku ikilenga kuongeza mauzo nje ya nchi. Hii inajumuisha utekelezaji wa Mpango wa Udhibiti wa Mabaki ya Kemikali na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Ubora wa Asali, ambao unalenga kuhakikisha asali ya Tanzania inakidhi viwango vya kimataifa na inavutia wateja wa kimataifa, hivyo kuimarisha ushindani na kuongeza Pato la Taifa.

Sambamba na hilo amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wafugaji nyuki na wafanyabiashara kwa kutoa msamaha wa VAT kwenye vifaa na mashine zinazohusiana na ufugaji na usindikaji wa mazao ya nyuki. Msamaha huu, ulioanzishwa kupitia Sheria ya Msamaha wa Kodi Na. 10 na Sheria ya Fedha Na. 6 ya mwaka 2024, unalenga kuongeza uzalishaji na mauzo ya asali nje ya nchi.

“Serikali imeanzisha utaratibu maalum kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kupata msamaha huu, na inahimiza wawekezaji kuchangamkia fursa hii,” anasema.

Kwa upande wake Waziri na Katibu wa Kamati ya CPC ya Utawala Mkuu wa Forodha ya Watu wa Jamhuri ya China Yu Jianhua amesema soko la China lina zaidi ya watu bilioni 1.4, na kila mwaka nchi hiyo inaagiza zaidi ya tani milioni 38 za asali. 

“Hii inamaanisha kuwa kuna fursa kubwa kwa Tanzania kupata mapato makubwa kupitia biashara ya asali na bidhaa nyingine za nyuki,” anasema.

JESHI LA POLISI LATOA TAMKO UTATA WA KIFO CHA MSANII MANDOJO.

JESHI LA POLISI LATOA TAMKO UTATA WA KIFO CHA MSANII MANDOJO.

RC CHALAMILA AIPONGEZA TPDC KWA KUTOA ELIMU YA UTUNZAJI MIUNDOMBINU YA SHIRIKA HILO.

RC CHALAMILA AIPONGEZA TPDC KWA KUTOA ELIMU YA UTUNZAJI MIUNDOMBINU YA SHIRIKA HILO.

BENKI YA BIASHARA TANZANIA (TCB) KUSHIRIKIANA NA  BUNGE LA TANZANIA KUWAINUA WAJASIRIAMALI NCHINI.

BENKI YA BIASHARA TANZANIA (TCB) KUSHIRIKIANA NA BUNGE LA TANZANIA KUWAINUA WAJASIRIAMALI NCHINI.

REA YAAHIDI KUENDELEA KUWAWEZESHA WAENDELEZAJI BINAFSI WA UMEME NCHINI.

REA YAAHIDI KUENDELEA KUWAWEZESHA WAENDELEZAJI BINAFSI WA UMEME NCHINI.

BASHUNGWA KUSIMAMIA MAELEKEZO YA DKT. NCHIMBI, BARABARA INAYOUNGANISHA KAGERA - KIGOMA KUKAMILIKA OKTOBA, 2024

BASHUNGWA KUSIMAMIA MAELEKEZO YA DKT. NCHIMBI, BARABARA INAYOUNGANISHA KAGERA - KIGOMA KUKAMILIKA OKTOBA, 2024