DCEA YAFANYA OPARESHENI MAALUM YA SIKU TISA MKOANI MOROGORO. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Kijamii

DCEA YAFANYA OPARESHENI MAALUM YA SIKU TISA MKOANI MOROGORO.

MAMLAKA ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni maalum mkoani Morogoro kwa muda wa siku tisa katika vijiji vya Nyarutanga, Lujenge na Mafumbo vilivyopo wilaya za Morogoro vijijini na Kilosa.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
26 Aug 2024
DCEA YAFANYA OPARESHENI MAALUM YA SIKU TISA MKOANI MOROGORO.

Katika vijiji vya mafumbo na Lujenge Mamlaka imeteketeza jumla ya ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi.

Aidha, katika operesheni iliyofanyika kijiji cha Nyarutanga  watu 6 wakiwa na kilogramu 342 za bangi wamekamatwa na watafikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Akizungumza mara baada ya utekelezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa mto  Mbakana,  Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.

 

“Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili. Pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa mito hiyo inatiririsha maji katika bwawa la Mwakimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme” amesema Lyimo.

 

Kadhalika, amewashukuru sana wananchi hususan vijana waliojitolea kushiriki katika zoezi zima la utekelezaji wa mashamba ya bangi pamoja na  Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha mamlaka kuweza kufanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kutokomeza dawa za kulevya nchini Tanzania.

 

“Sisi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tutajitahidi kutekeleza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha kwamba tunamaliza tatizo la dawa za kulevya nchini ikiwemo mashamba ya bangi, mashamba ya mirungi pamoja na kudhibiti kemikali bashirifu na matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kutumika kama mbadala wa dawa za kulevya.  Hivyo, wote watakaojihusisha na uzalishaji, matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya tutawakamata” amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.

 

Hata hivyo, amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine kushirikiana na Mamlaka kupiga vita kilimo cha bangi na aina nyingne za dawa za kulevya kwa ujumla kwani operesheni hizi ni endelevu.

 

Kwa upande wake Saidi Mijinga mkazi wa Kisaki, na mmoja wa vijana waliojitolea kishirikiana na Mamlaka kufyeka mashamba ya bangi amesema, eneo lililotumika kulima bangi ni kubwa sana, endapo lingetumika kulima mazao mengine  wananchi wangenufaika kwani mazao hayo hulimwa bila kificho na kuuzwa kwa uwazi jambo ambalo lingewaletea faida ya chakula na kipato na  hivyo, kuondokana na changamoto za njaa kwani kuna wakati wanakumbwa na tatizo hilo.

 

“Ninawashauri wanaolima bangi waache hii tabia walime mazao mengine ili tufaidike wote kwa sababu kuna kunde, mahindi, choroko, maharage na mbaazi  yote haya yanakubali. Hili eneo ni kubwa sana linaweza likatulisha sisi kijiji na kuifanya njaa isiwe gumzo. Kwani kuna muda unafikaga vyakula hakuna zipo bangi tu, Sisi hatuwezi kula bangi” amesema.

 

Naye Joseph Juma Kibaya mkazi wa Nyarutanga amewaomba wananchi waendelee kuwafichua wauzaji na wafanyabiasha wa bangi kwani inamadhara makubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla, na kuomba raia waungane na kuwa kitu kimoja kupinga bangi ili kuepuka athari zake kwa vijana na vizazi vya baadaye.

 

EKARI 1,165 za mashamba ya bangi zateketezwa Morogoro

EKARI 1,165 za mashamba ya bangi zateketezwa Morogoro

FCS KUADHIMISHA WIKI YA AZAKI SEPTEMBA 9,ARUSHA.

FCS KUADHIMISHA WIKI YA AZAKI SEPTEMBA 9,ARUSHA.

JAMII YA KIMASAI IMEANZA KUENDANA NA KASI YA UTANDAWAZI.

JAMII YA KIMASAI IMEANZA KUENDANA NA KASI YA UTANDAWAZI.

TBS YAFUNGUA MASHINDANO YA TUZO ZA UBORA KITAIFA.

TBS YAFUNGUA MASHINDANO YA TUZO ZA UBORA KITAIFA.

FCS YAIOMBA SERIKALI KUWAWEZESHA MAKUNDI MAALUM MIUNDOMBINU YA KIDIGITAL

FCS YAIOMBA SERIKALI KUWAWEZESHA MAKUNDI MAALUM MIUNDOMBINU YA KIDIGITAL