Dodoma yazindua mkakati wa utalii huku serikali ikitaka utekelezaji wa vitendo unaolenga kuiweka mkoa huo kwenye ramani ya dunia ya utalii. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Utalii

Dodoma yazindua mkakati wa utalii huku serikali ikitaka utekelezaji wa vitendo unaolenga kuiweka mkoa huo kwenye ramani ya dunia ya utalii.

Katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kuendeleza Utalii wa Mkoa wa Dodoma, serikali imesisitiza kuwa huu si wakati wa maandiko ya mipango pekee, bali ni hatua ya utekelezaji unaopaswa kuibadilisha Dodoma kiuchumi na kijamii.

Moreen Rojas, Dodoma
By Moreen Rojas, Dodoma
21 Aug 2025
Dodoma yazindua mkakati wa utalii huku serikali ikitaka utekelezaji wa vitendo unaolenga kuiweka mkoa huo kwenye ramani ya dunia ya utalii.

Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, alisema mkakati huo ni sehemu ya majibu kwa kiu ya muda mrefu ya kuitangaza Dodoma kimataifa kupitia vivutio vyake vya kipekee.

Mhe. Jafo alieleza kuwa Tanzania imebarikiwa vivutio vya asili, historia na utamaduni vinavyoweza kutumika kama nyenzo ya kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii.

Alisisitiza kuwa bidhaa kama mchuzi wa zabibu, mvinyo wa asili, historia ya wapigania uhuru na maeneo ya urithi wa taifa ni turubai ya kuiweka Dodoma kwenye ramani ya dunia. “Mkakati huu si tu waraka wa maono, bali ni chombo cha mageuzi kwa mkoa huu,” alisema.

Akibainisha nafasi ya miundombinu katika kufanikisha lengo hilo, Waziri Jafo alisema serikali inatarajia kukamilisha kwa wakati ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambao utakuwa lango la moja kwa moja kwa watalii wanaoingia kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa SGR na maeneo yanayozunguka vituo vya treni kuandaliwa kitalii ili kutoa taswira ya mkoa wenye utambulisho wa kiutamaduni na kiutalii kwa wageni wa ndani na nje.

Katika kuendeleza urithi wa asili, Jafo alipendekeza kuanzishwa kwa kijiji cha utalii wa Wagogo kitakachohifadhi na kuonyesha nyimbo, mavazi, mapishi na maisha ya jadi. “Utalii unaanza na wewe,” aliongeza, akisisitiza kuwa kila mwananchi anayo nafasi ya kuwa balozi wa utalii kwa kuenzi, kutunza na kutangaza vivutio vya eneo lake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alisema mkakati huo umejengwa katika msingi wa kuitumia kaulimbiu ya “Ipeleke Dodoma Kimataifa, Ilete Dunia Dodoma” kwa vitendo.

Alisema mkoa huo unazo rasilimali nyingi za asili na historia ambazo bado hazijatumika ipasavyo, ikiwemo misitu ya hifadhi ya Swagaswaga na Mkungunero, historia ya Kongwa kama makazi ya wapigania uhuru, pamoja na majengo ya kihistoria kama Ikulu ya zamani na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Senyamule alisisitiza kuwa utalii wa kilimo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa kwa Dodoma, akieleza kuwa zabibu na mashamba yake yanaweza kutumika kama vivutio vya kipekee kwa watalii wa ndani na nje, wajasiriamali na watafiti. Aliongeza kuwa mapishi ya kienyeji, mavazi ya asili, lugha na tamaduni za Wagogo, Warangi, Wasandawe na Waburunge ni hazina ambayo inapaswa kutumika kama bidhaa ya kitalii.

Aidha, alieleza kuwa mkakati huo unahitaji mshikamano wa wadau wote wakiwemo sekta binafsi, viongozi wa serikali, vijana na jamii kwa ujumla. “Hii si kazi ya serikali peke yake. Tunahitaji kila mdau kushiriki kwa vitendo katika kuijenga Dodoma mpya – mji wa urithi, fursa na utalii endelevu,” alisema.

Katika kuhakikisha mafanikio ya mkakati huo, serikali imesema itaendelea kuweka miundombinu wezeshi, kurahisisha mifumo ya uwekezaji, kutoa vibali kwa wakati na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wote wa sekta ya utalii.

TAWA YATUMIA MAONESHO YA 31 YA NANE NANE 2025  KUELIMISHA UMMA NA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

TAWA YATUMIA MAONESHO YA 31 YA NANE NANE 2025 KUELIMISHA UMMA NA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

ARUSHA YAJIVUNIA ONGEZEKO LA WATALII KUPITIA FILAMU YA THE  ROYAL TOUR.

ARUSHA YAJIVUNIA ONGEZEKO LA WATALII KUPITIA FILAMU YA THE ROYAL TOUR.

AJIRA ZA MOJA KWA MOJA KATIKA SEKTA YA UTALII ZIMEONGEZEKA.

AJIRA ZA MOJA KWA MOJA KATIKA SEKTA YA UTALII ZIMEONGEZEKA.

IDADI YA WATALII WA NDANI WALIOTEMBELEA MKOA WA TABORA IMEONGEZEKA.

IDADI YA WATALII WA NDANI WALIOTEMBELEA MKOA WA TABORA IMEONGEZEKA.