REA YASAINI MIKATABA YA KUPELEKA UMEME KWENYE VITONGOJI 3,060 KOTE NCHINI | The Dodoma Post
The Dodoma Post Nishati

REA YASAINI MIKATABA YA KUPELEKA UMEME KWENYE VITONGOJI 3,060 KOTE NCHINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Mashaka Biteko leo, tarehe 20 Agosti, 2024 ameshuhudia tukio kubwa la kihistoria baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusaini mikataba ya kupeleka nishati ya umeme kwenye vitongoji 3,060 vya Tanzania Bara, tukio liliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

Moreen Rojas, Dodoma.
By Moreen Rojas, Dodoma.
20 Aug 2024
REA YASAINI MIKATABA YA KUPELEKA UMEME KWENYE VITONGOJI 3,060 KOTE NCHINI

“Kipekee ninaipongeza Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa juhudi kubwa ya kuhamasisha, uwekezaji na uwezeshaji wa upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya vijijini, sisi sote ni mashahidi kuwa vijiji vyetu vimekuwa na kasi ya maendeleo kutokana na uwepo wa umeme unapolekwa kupitia Miradi inayotekelezwa na REA”.

“Tunafahamu kuwa Wakala (REA) upo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha safari ya kupelekea umeme vijijini, na kama tulivyofahamishwa, vijiji vilivyosalia, ambavyo havijafikiwa na umeme ni 151 ambapo inatarajiwa hadi tarehe 30 Septemba, 2024 viwe vimekamilika, kwa sasa Serikali inahama kutoka kwenye kupeleka umeme kwenye vijiji hadi kwenye vitongoji, jambo ambalo safari yake ndiyo imeanza leo.” Amekaririwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko.


Dkt. Biteko ameongeza kuwa, Mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji utatekelezwa kwa awamu ambapo, leo inashuhudiwa vitongoji takribani 3,060 vitapatiwa umeme kupitia mradi huu kwa gharama ya Jumla ya bilioni 362.

“Kwa takribani miaka 17 hadi sasa, Serikali imekuwa ikishirikiana na Wabia wa Maendeleo katika utekelezaji miradi mbalimbali ya kimkakati ya nishati vijijini.” Amesema Dkt. Biteko.

"Mikataba hii tuliyoishudia leo yenye jumla ya shilingi bilioni 362.8 imewezeshwa kupitia ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, naomba niwashukuru Washirika wa Maendeleo wanaochangia katika mfuko wetu wa Nishati Vijijini, hususan Benki ya Dunia, Serikali za Norway na Sweden, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)," amesema Dkt. Biteko.

"Wananchi wanatarajia kunufaika na mradi huu wanayo matarajio makubwa kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme utaboresha na kuinua hali zao za maisha kupitia ushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Niwahakikishie Wananchi wote kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha, na kushirikiana na wabia wa maendeleo kuhakikisha kuwa umeme unawafikia Watanzania wote, popote walipo, " ameongeza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dkt. David Mathayo David ameipongeza Serikali kwa juhudi za makusudi za kusambaza umeme kwenye vitongoji 3,060 jambo ambalo linakwenda kutekelezwa sasa na REA.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, amesema hadi kufikia Desemba 2024, vijiji vyote vya Tanzania Bara 12,318 vitakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme, hatua ambayo itaongeza hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

Mhandisi Hassan Saidy amesema pamoja na mafanikio makubwa ya kupeleka umeme katika vijiji vyote nchi nzima, bado takribani vitongoji 31,532 sawa na asilimia 49 havijafikiwa na huduma ya umeme.

“Mpango wa Serikali kupitia Wakala ni kufikisha umeme kwenye vitongoji 13,000 katika miaka mitatu ijayo, tukianza na vitongoji 3,060 ambavyo mikataba ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji hivyo inasainiwa leo”. Amesema Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy.

Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa mikataba iliyosainiwa leo, tarehe 20 Agosti, 2024 itahusisha ujenzi wa njia za msongo wa kati wa umeme zenye urefu wa km258, ujenzi wa njia za msongo mdogo wa umeme zenye urefu wa km6118, ufungaji transfoma 3,059 pamoja na kuunganisha wateja takribani laki moja (100,000), hatua ambayo itaongeza uunganishwaji wa Wananchi na huduma za umeme kwa gharama za takribani bilioni 362.

Wakati huo huo, Mhandisi Saidy aliwakumbusha Wakandarasi 13 walioshinda zabuni ya kusambaza umeme kwenye vitongoji kuzingatia muda wa utekelezaji wa Mradi ambao ni miezi ishirini na nne (24) na siku kumi na nne (14) baada ya kusaini mikataba; kufanya kazi na Viongozi wa Serikali za Vijiji, Vitongoji hadi Wilaya, kwa sababu Miradi hiyo yote ni ya Wananchi.

Mhandisi, Saidy amewakumbusha pia Wakandarasi kutoa taarifa kwenye maeneo yote watakapokwenda kutekeleza Miradi hii ili kupata ridhaa ya Viongozi na Wananchi hususan kwenye maeneo ambayo yatakayohitaji kukata miti au mazao mashambani, ni lazima wapate ridhaa kwa kuwa Miradi ya kupelekea nishati kwenye Vitongoji haina fidia.

Aidha, amewakumbusha wakati wanapokwenda kufanya “survey” kwa ajili ya kuandaa michoro na wigo wa kazi, wahakikishe michoro na wigo wa kazi unakuwa hauna utofauti ule uliopo kwenye Mradi ili kuepuka utofauti (Variation).

BRIGEDIA Jenerali Ngata Apongezwa uongozi makini SUMAJKT

BRIGEDIA Jenerali Ngata Apongezwa uongozi makini SUMAJKT

KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAAHIDI KUUPA MSUKUMO MRADI WA EACOP

KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAAHIDI KUUPA MSUKUMO MRADI WA EACOP

WIZARA YA NISHATI IPO KWENYE MCHAKATO WA KUZALISHA MBOLEA KWA KUTUMIA GESI ASILIA.

WIZARA YA NISHATI IPO KWENYE MCHAKATO WA KUZALISHA MBOLEA KWA KUTUMIA GESI ASILIA.