Kilimo Ni Mhimili wa Uchumi wa Tanzania Kikichangia Asilimia 26.5 ya Pato la Taifa. | The Dodoma Post
The Dodoma Post Biashara

Kilimo Ni Mhimili wa Uchumi wa Tanzania Kikichangia Asilimia 26.5 ya Pato la Taifa.

Kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania kikichangia asilima 26.5 ya Pato la Taifa, kimeajiri takribani asilimia 65 ya nguvukazi nchini, na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje ya nchi.

Moreen Rojas,Dodoma
By Moreen Rojas,Dodoma
21 Oct 2025
Kilimo Ni Mhimili wa Uchumi wa Tanzania Kikichangia Asilimia 26.5 ya Pato la Taifa.

Kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania kikichangia asilima 26.5 ya Pato la Taifa, kimeajiri takribani asilimia 65 ya nguvukazi nchini, na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje ya nchi.

Sekta hii ina uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na kuchochea ongezeko la mapato kupitia mauzo ya mazao na bidhaa zinazotokana na mazao hayo,Aidha, pamoja na mafanikio haya, wakulima na wazalishaji wadogo wanahitaji ujuzi hususan katika uongezaji wa thamani wa mazao.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Bi.Zuhura Yunus Leo katika Uzinduzi wa Mafunzo ya Kuongeza ujuzi kwa Wakulima na wasindikaji wadogo katika Sekta ya Kilimo jijini Dodoma.

Aidha amesema Serikali itahakikisha mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Taifa unaongezeka kutoka asilimia 4.6 mwaka 2025 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 kwa  kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula, kuongeza kipato cha wakulima, kukuza pato la Taifa, ili kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda, na kuongeza ajira.

Aidha, Serikali itaanzisha mfuko wa dhamana kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Ushirika ili kuwawezesha wakulima na wananchi wengine wanaojishughulisha na uongezaji wa thamani kwa mazao ya kilimo, mifugo na samaki kukopa katika taasisi za fedha kwa riba ndogo.

"Katika kipindi cha Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeshuhudia mageuzi makubwa na mafanikio ya hali ya juu katika Sekta ya Kilimo, mfano programu ya “Building a Better Tomorrow” inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ambayo inalenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kwenye kilimo cha kibiashara, kutoa mafunzo ya kitaalamu ya kilimo na ujasiriamali, kuboresha upatikanaji wa teknolojia na miundombinu ya kilimo, kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo kwa kuifanya kuwa ya kisasa, yenye faida, na endelevu"Amesema Bi. Zuhura

"Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imekusudia kuwa, ifikapo mwaka 2050 uchumi wa Tanzania utakuwa shindani na mseto, unaotegemea viwanda huku ukichagizwa na nguvukazi yenye maarifa na ujuzi. Ili kufanikisha lengo hili,

"Serikali imeendelea kushirikiana na wadau kutoka sekta  ya umma na binafsi kuwezesha nguvukazi katika sekta mbalimbali kupata ujuzi stahiki kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.  Katika mwaka huu wa fedha 2025/2026, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imepanga kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi yaani “Up-skilling training” kwa wakulima na wazalishaji wadogo wapatao 1,000 katika sekta ya kilimo"Amesisitiza Bi. Zuhura

Sanjari na hayo amesema Mafunzo haya yatatolewa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha njia za utendaji kazi ili kuongeza ubora wa bidhaa na kutoa huduma bora zaidi katika sekta ya kilimo. Mafunzo haya yatawezesha kuongezeka kwa ujuzi, kipato binafsi, kuongezeka kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali na kukuza pato la taifa.

Aidha kwa mwaka huu 2025/26 mafunzo haya yanatolewa katika Mikoa minne ya Dodoma, Singida, Iringa na Mbeya ambapo yamejikita zaidi katika mafunzo ya vitendo ili kuwawezesha washiriki kuona moja kwa moja kinachofundishwa na kuelekezwa, hivyo kuweza kufanya mazoezi wenyewe.

Katika mafunzo hayo, mazao yatakayohusika katika mafunzo ni zabibu kwa Mkoa wa Dodoma, alizeti kwa Mkoa wa Singida, nyanya na mchicha lishe kwa mkoa wa Iringa, maharage na parachichi, pamoja na matumizi ya mashine na mitambo ya kilimo kwa mkoa wa Mbeya.

"Hivyo, napenda kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza ujuzi ili kupanua wigo wa kufikia wakulima na wazalishaji wadogo wengi zaidi katika sekta ya kilimo"

Kwa upande wake katibu Tawala Msaidizi Dodoma sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Bi.Aziza Muumba amesema zabibu ni zao la kimkakati linalotoa ajira kwa watu wengi kwani mnyororo wake wa thamani ni mkubwa mno.

Aidha amewasihi wakulima kuangalia vigezo na masharti wanayo fundishwa ili kuweza kuleta chakula salama kwa wananchi.

"Natamani sana wakulima tungekuwa na umoja watu ili kuweza kufanya mambo yetu kuwa marahisi na kuweza kuwafikia wakuu wa Idara mbalimbali na kutatua changamoto zetu"Amesema Bi.Aziza

Naye mmoja wa wanufaika wa Mafunzo hayo Mnoha Majeje amesema anaishukuru ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kuweza kuwapatia Mafunzo hayo kwani yatawasaidia kujikwamua kiuchumi na kufanya kilimo Cha kisasa na chenye tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Thomas Bwana ambaye anaongoza timu ya wataalam kufundisha wakulima hao ameshauri kuwa watumie elimu na  ujuzi watakao upata Kwenda kuwafundisha wenzao ili tija inayokusudiwa iweze kupatikana.

Dkt. Bwana ameongeza kwa kusema kuwa TARI imejipanga kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya zinawafikia na kuwasaidia wakulima na wasindikaji wa bidhaa za kilimo nchini ili tija ipatikane na kuchangia ukuaji wa Uchumi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Alana Nchimbi alieleza kuwa mafunzo hayo baada ya kufunguliwa leo yatatolewa katika mikoa minne na aina mazao yatakayohusika kwenye mafunzo hayo ni Dodoma (zabibu), Singida (alizeti), Iringa (nyanya na mchicha lishe) na Mbeya (maharage na parachichi) ambapo jumla ya wakulima 250 kwenye mikoa hiyo watanufaika.

Alana aliongeza kuwa Ofisi hiyo inaratibu mafunzo hayo kwa kushirikana na wadau ili kuwezesha nguvukazi katika sekta mbalimbali kupata ujuzi stahiki kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Up-Skilling training) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

FCC  YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

FCC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

DC Nyamwese aanika fursa za uwekezaji Handeni

DC Nyamwese aanika fursa za uwekezaji Handeni

Nala Dodoma Kuwa Kitovu cha Viwanda, Wawekezaji Wajitokeza

Nala Dodoma Kuwa Kitovu cha Viwanda, Wawekezaji Wajitokeza

CRDB WATOA GARI LA PILI KWA MSHINDI,WATANZANIA WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA.

CRDB WATOA GARI LA PILI KWA MSHINDI,WATANZANIA WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA.

Kodi Sasa Si Kikwazo: Wafanyabiashara Wazidi Kuunga Mkono Serikali.

Kodi Sasa Si Kikwazo: Wafanyabiashara Wazidi Kuunga Mkono Serikali.