Huduma za Uwakala CRDB Zachochea Ukuaji wa Mapato ya Serikali na Ujumuishi wa Kifedha | The Dodoma Post
The Dodoma Post Tanzania

Huduma za Uwakala CRDB Zachochea Ukuaji wa Mapato ya Serikali na Ujumuishi wa Kifedha

Zaidi ya miamala milioni 200 yenye thamani ya Shilingi trilioni 70 imefanyika kupitia mawakala wa Benki ya CRDB nchini kote ndani ya mwaka mmoja, hatua inayotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa mapato ya Serikali na kupanua wigo wa ujumuishi wa kifedha nchini.

Sophia Kingimali
By Sophia Kingimali
13 Oct 2025
Huduma za Uwakala CRDB Zachochea Ukuaji wa Mapato ya Serikali na Ujumuishi wa Kifedha

Zaidi ya miamala milioni 200 yenye thamani ya Shilingi trilioni 70 imefanyika kupitia mawakala wa Benki ya CRDB nchini kote ndani ya mwaka mmoja, hatua inayotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa mapato ya Serikali na kupanua wigo wa ujumuishi wa kifedha nchini.

Takwimu hizo zimebainishwa jijini Dar es Salaam leo Octoba 13,2025 na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki hiyo, Muhinuliza Buberwa, wakati wa semina ya mawakala wa CRDB wilaya ya ubungo, ambapo zaidi ya Shilingi trilioni 3 kati ya kiasi hicho ni makusanyo ya Serikali yaliyopokelewa kupitia mfumo wa uwakala.

Buberwa amesema matokeo hayo yanadhihirisha mafanikio ya sera za nchi katika kuhimiza matumizi ya huduma za kifedha jumuishi, hususan kupitia mifumo ya kidijitali, ambayo imekuwa chachu ya kuongeza mapato ya Serikali na kukuza biashara katika ngazi ya jamii.

“Huduma za uwakala zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kifedha. Hivi sasa hakuna tofauti kati ya mteja anayetembelea tawi la benki na anayehudumiwa na wakala wetu, kwa sababu huduma zote muhimu zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu,” amesema Buberwa.

Aidha, amesema benki hiyo imezindua huduma bunifu ijulikanayo kama Tokenization, itakayowawezesha wateja wa CRDB, hata wale wasio na akaunti, kutoa fedha walizotumiwa kupitia wakala yeyote wa CRDB bila kutozwa gharama ya ziada.

 “Tokenization inamwezesha mteja kutuma pesa kwa mtu yeyote, bila kujali kama ana akaunti ya CRDB au la. Mpokeaji hupokea ujumbe wenye namba ya siri (code) ambayo humuwezesha kuchukua fedha kwa wakala yeyote wa CRDB nchini,” amefafanua Buberwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawakala na Huduma za Malipo wa CRDB, Catherine Lutenge, amesema semina hiyo imehusisha zaidi ya mawakala 800 kutoka Wilaya ya Ubungo na inalenga kuwajengea uwezo mawakala katika matumizi bora ya mifumo ya kidijitali, hasa mashine za POS, ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Mawakala walioshiriki walipongeza hatua hiyo wakisema elimu waliyopata itawasaidia kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi na kuongeza wigo wa watumiaji wa huduma za kifedha katika maeneo ya vijijini na mijini.

Kwa sasa Benki ya CRDB ina zaidi ya mawakala 45,000 nchi nzima, sawa na asilimia 55 ya mawakala wote wa huduma za kifedha nchini, jambo linaloifanya kuwa kinara katika kutoa huduma kupitia mtandao wa uwakala.

HAKUNA LITAKALOTOKEA OKTOBA 29, NENDENI MKAPIGE KURA- MSIGWA

HAKUNA LITAKALOTOKEA OKTOBA 29, NENDENI MKAPIGE KURA- MSIGWA

TUKACHAGUE VIONGOZI TUWATAKAO KUEPUSHA LAWAMA NA MALALAMIKO

TUKACHAGUE VIONGOZI TUWATAKAO KUEPUSHA LAWAMA NA MALALAMIKO

Vijana sasa kujifunza ufundi kwa urahisi kupitia programu ya  VSOMO ya VETA

Vijana sasa kujifunza ufundi kwa urahisi kupitia programu ya VSOMO ya VETA

WENYE ULEMAVU WAHAMASISHA KUJITOKEZA KUWACHAGUA VIONGOZI WANAOWEZA KUTETEA MASLAHI YAO

WENYE ULEMAVU WAHAMASISHA KUJITOKEZA KUWACHAGUA VIONGOZI WANAOWEZA KUTETEA MASLAHI YAO

BRIGEDIA JENERALI NDAGALA AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA USIMAMIZI WA MAAFA JIJINI MBEYA

BRIGEDIA JENERALI NDAGALA AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA USIMAMIZI WA MAAFA JIJINI MBEYA