

JUMLA ya watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita unaotarajiwa kufanyika Mei, 5(leo) hadi 26 mwaka huu, nchini
JUMLA ya watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita unaotarajiwa kufanyika Mei, 5(leo) hadi 26 mwaka huu, nchini.
Katika mtihani huo watahiniwa wa shule ni 126,957 na wakujitegemea ni 7,433.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dk.Said Mohamed alisema kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa , wanaume ni 64,581 sawa na asilimia 50.87 na wasichana ni 62, 376 sawa na asilimia 49.13.
Pia watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 453 ambao kati yao 300ni wenye uoni hafifu, 16 wasioona , 75 wenye ulemavu wa viungo vya mwili , wenye ulemavu wa akili wanne na wenye uziwi 58.
Alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 7,433 wamesajiliwa, wavulana ni 4782 sawa na asilimia 64.33 na wasichana ni 2,651 sawa na asilimia 35.67 huku mtahiniwa wa kujitemea wenye mahitaji maalumu wakiwa 151 kati yao wenye uoni hafifu ni 142 na wasioona ni tisa.
Alisema kumekuwa na ongezeko la jumla la watahiniwa wa shule na kujitegemea 20,854 sawa na asilimia 18.37 mwaka huu ukilinganisha na mwaka 2024 ambapo walikuwa 113,536.
"Katika mtihani wa ualimu, unaotarajia kuanza Mei 5, hadi 19, mwaka huu , jumla ya watahiniwa 10,895 wamesajiliwa na kati yao 3100 ni ngazi ya stashahada na watahiniwa 7775 ni ngazi ya cheti, Kwa ngazi ya stashahada wanaume ni 1751 sawa na asilimia 56.48 na wanawake ni 1349 sawa na asilimia 43.52," alisema.
Pia, watahiniwa 3808 wa ngazi ya cheti sawa na asilimia 48.85 ni wanaume na watahiniwa 3987 sawa na asilimia 51.15 ni wanawake, watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosajiliwa kufanya mtihani wa ualimu ni 23 kati yao wawili ni wenye uoni hafifu kwa ngazi ya stashahada na 16 wenye uoni hafifu, watatu wasioona, mwenye uziwi mmoja na ulemavu wa viungo ngazi ya cheti ni mmoja.
Alisema mwaka 2024, idadi ya watahiniwa wa ualimu waliosajiliwa walikuwa 11, 435 hivyo kuna upungufu wa jumla ya watahiniwa 540 sawa na asilimia 4.72 kwa mwaka huu.
Alisema maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika ikiwa kusambaza mitihani husika, vitabu vya kununua na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika Mikoa na Halmashauri.
Dk.Mohamed alisema mtihani huo ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, kwani hupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi katika maeneo yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka miwili.
Pia baraza hilo limezitaka kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, Manispaa na majiji kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji zinazingatiwa.
" Kamati zihakikishe mazingira ya mitihani yanakuwa salama, tulivu na kuzuia mianya yote inavyoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu, kuimarisha usalama wa vituo teule na kuvisimamia kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza hilo,"alisema.
Pia aliwataka wasimamizi wa Mitihani kufanya kazi kwa kusimamia Mitihani kwa kwa welidi na uaminifu wa hali ya juu kwa kuzingatia kanuni za mtihani, taratibu na miongozo ya Baraza la Mitihani waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake.
Katibu huyo alisema anaamini kuwa walimu na wakufunzi wamewaandaa vizuri katika miaka miwili ya elimu ya sekondari ya juu na kozi ya mafunzo ya ualimu, hivyo anatarajia kila mtahiniwa atafanya mtihani kwa kuzingatia kanuni za mtihani.
" Baraza halitarajii kuona mtahiniwa yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, mtahiniwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.
Pia NECTA imewataka wakuu wa shule na wakuu wa vyuo kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi uliotolewa ba baraza na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mtihani kwani halitasita kukifutia kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mtihani.
"Baraza halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na kusababisha udanganyifu kufanyika kwa mujibu wa sheria za nchi, alisema.
Hata hivyo mtihani wa kidato cha sita unatarajiwa kufanyika katika jumla ya shule za sekondari 982 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 245 na mtihani wa ualimu utafanyika katika vyuo vya ualimu 68.
=======
Rais Samia Asisitiza Mchujo wa Wagombea Kufanyika Kwa Haki.
Ilani Ya CCM Imeandaliwa Kwa Weledi Mkubwa Kwa Kushirikiana Na Wananchi;RAIS Dkt.Samia
WIZARA YA ARDHI YAJA NA VIPAUMBELE SABA
SERIKALI NA WADAU WAENDELEZA MAPAMBANO YA KIJINSIA
KAPINGA ATAJA VIGEZO VYA ZIADA UPELEKAJI UMEME VITONGOJINI.