Wasichana waaswa kutumia mitandao kwa manufaa | The Dodoma Post
The Dodoma Post Kijamii

Wasichana waaswa kutumia mitandao kwa manufaa

WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Balozi Liberata Mulamula amewahimiza wasichana kuwa makini wanapotumia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa mitandao hiyo inaweza kuwa na manufaa makubwa ya kuwaelimisha na kuwaunganisha na dunia, lakini pia inaweza kuwa na athari hasi ikiwa haitatumika kwa uangalifu.

The Dododma Post
By The Dododma Post
12 Oct 2024
Wasichana waaswa kutumia mitandao kwa manufaa

Akizungumza leo jijini Dodoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku hiyo, Balozi Mulamula alisema kuwa mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa kwa njia chanya kama vile kuongeza ujuzi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Hata hivyo, alionya kuwa mitandao hiyo inaweza kuwa na athari hasi inapokuwa na maudhui yanayokinzana na maadili na mila za Kitanzania.

"Teknolojia ya kidijitali imekuwa chombo muhimu kinachowawezesha wasichana kufikia malengo yao na kujenga jamii bora hivyo ni wakati sasa wasichana kuanza kutumia mitandao kwa manufaa, kama vile kupata elimu na kujifunza kuhusu uongozi, badala ya kutumia kwa mambo yasiyofaa."

Akizungumzia Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Balozi Liberata alieleza kuwa siku hiyo, iliyoanzishwa rasmi mwezi Septemba mwaka 2011, inaadhimishwa kwa mara ya nane mwaka huu.

Alieleza kufurahishwa na kaulimbiu ya mwaka huu, “Msichana na Uongozi Kupitia Nguvu ya Teknolojia ya Kidijitali,”inalenga kuwahamasisha wasichana kote ulimwenguni kutumia teknolojia ili kuimarisha uwezo wao wa uongozi na kuchangia maendeleo ya jamii.

“Hapo zamani, mtoto wa kike mara nyingi alionekana kama mtu dhaifu na alitarajiwa tu kuwa mama wa nyumbani,” alisema. “Hata hivyo, maendeleo ya sasa yameleta mabadiliko makubwa; wasichana wanapata fursa za kujitambua, kujifunza, na kuelewa jinsi dunia inavyobadilika, hasa kupitia majukwaa ya kidijitali.”

Dkt. Majaliwa Malwa, msaidizi wa mwakilishi mkazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), naye alisisitiza umuhimu wa Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. Alisema siku hii inatoa fursa ya kujadili changamoto, mafanikio, na fursa zinazohusiana na mtoto wa kike.

Aliongeza kuwa uongozi na teknolojia ni nyenzo muhimu kwa wasichana, na endapo watawezeshwa kwa elimu, stadi za maisha, na huduma bora za afya ya uzazi, wataweza kufikia ndoto zao na kutoa mchango mkubwa katika jamii na taifa kwa ujumla.

Alibainisha kuwa UNFPA, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inafanya kazi kuhakikisha ndoto za wasichana zinafikiwa huku serikali ikitekeleza sera na mipango mbalimbali.

"Mwaka huu, serikali imezindua sera ya jinsia pamoja na toleo jipya la sera ya vijana mwezi Agosti, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha haki na usawa kwa watoto wa kike na vijana. Pia, tumeendelea kushirikiana na wadau kutoa mafunzo kwa watoa huduma wanaoshughulikia watoto wa kike na vijana," alisema Dkt. Malwa.

Kwa upande wake, Furaeni Michael, Meneja wa Miradi kutoka shirika la Msichana Initiative, ambalo linaratibu kikao cha “Agenda ya Msichana,” alisema kuwa wameweza kufikia zaidi ya wasichana 6,000 katika mikoa mbalimbali.

Alisema kuwa juhudi hizo zinawalenga wasichana na kuwajengea uwezo wa kujitambua, kuthaminiwa, na kukubaliwa, ili waweze kufikia malengo yao na kuleta mabadiliko katika jamii licha ya changamoto zinazotokana na mila, tamaduni, na desturi katika jamii.
 

MPANGO KAZI KUKOMESHA MAUAJI YA WATU WENYE UALBINO WADAU WAIPONGEZA SERIKALI.

MPANGO KAZI KUKOMESHA MAUAJI YA WATU WENYE UALBINO WADAU WAIPONGEZA SERIKALI.

Wachimbaji wa Madini wahimizwa kulipa kodi ya Serikali.

Wachimbaji wa Madini wahimizwa kulipa kodi ya Serikali.

JAFO AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA NA FCC KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA UWEKEZAJI.

JAFO AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA NA FCC KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA UWEKEZAJI.

FDH YAIPONGEZA UNEP KUENDELEZA AGENDA YA MAZINGIRA KWA WENYE ULEMAVU

FDH YAIPONGEZA UNEP KUENDELEZA AGENDA YA MAZINGIRA KWA WENYE ULEMAVU

JAMII YAASWA KUTUMIA NISHATI SAFI ILI KUUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS SAMIA

JAMII YAASWA KUTUMIA NISHATI SAFI ILI KUUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS SAMIA