Serikali Yatangaza Kuanza Msako Kuwabaini Wanaotumikisha Watoto | The Dodoma Post
The Dodoma Post Siasa

Serikali Yatangaza Kuanza Msako Kuwabaini Wanaotumikisha Watoto

Utumikishwaji wa watoto umetajwa kuwa moja ya vikwazo vikuu vinavyodhoofisha maendeleo ya taifa, huku Serikali ikitangaza kuanza msako maalum wa kuwabaini waajiri wanaokiuka haki za watoto kwa kuwaingiza katika ajira zisizo rasmi na hatarishi.

Moreen Rojas, Dodoma
By Moreen Rojas, Dodoma
12 Jun 2025
Serikali Yatangaza Kuanza Msako Kuwabaini Wanaotumikisha Watoto

Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, ameyasema hayo Juni 12, 2025, jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji Watoto. Amesema kuwa taifa haliwezi kufikia maendeleo ya kweli bila kulinda haki na ustawi wa watoto.

“Ajira za watoto si tu kwamba zinavunja sheria, bali zinakata mnyororo wa matumaini kwa vizazi vijavyo. Tunachukua hatua kali kwa waajiri wote wanaokiuka haki hizi,” amesema Katambi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 haruhusiwi kabisa kufanya kazi ya kuajiriwa.

Hata hivyo, watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 wanaruhusiwa tu kufanya kazi nyepesi zisizoathiri afya yao, mahudhurio shuleni, au maendeleo yao ya kielimu na kimwili.

Waziri Katambi amebainisha kuwa Serikali imeongeza vifaa na magari kwa maofisa ukaguzi wa kazi ili kufanikisha udhibiti wa ajira haramu kwa watoto, hasa maeneo ya vijijini na katika sekta zisizosimamiwa ipasavyo kama kilimo, migodi na kazi za nyumbani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Groly Emmanuel, amesema kuwa zaidi ya watoto milioni 160 duniani wanatumikishwa, huku wengi wakijihusisha na kazi hatarishi, hasa katika kilimo.

“Mtoto wa kike bado anaathirika zaidi, hasa katika ajira za ndani ambazo mara nyingi hufanyika kwa siri na bila ulinzi wa kisheria,” alisema Emmanuel. Ameongeza kuwa asilimia 24.9 ya watoto hao wanahusika na kazi mbaya zaidi kama migodini, usafirishaji haramu na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Emmanuel ametoa wito kwa nchi wanachama wa ILO kuwekeza zaidi kwenye ajira zenye staha kwa wazazi, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ajira kwa watoto ili kuondoa utegemezi wa kipato kutoka kwao.

Naye Kamishna wa Kazi, Susan K. Mkangwa, amesema Serikali kupitia Idara ya Kazi imeanza maandalizi ya kaguzi maalum katika mashamba, migodini na maeneo ya kazi ili kubaini watoto wanaotumikishwa na kuwachukulia hatua waajiri wote wanaohusika.

“Tutazindua kampeni za kitaifa za uelimishaji ili kuifikia jamii moja kwa moja. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mtoto anayepoteza haki yake ya elimu na utoto kwa sababu ya tamaa ya kipato cha haraka,” amesema Kamishna Mkangwa.

Maiko Salali Arejesha Fomu ya Kugombea Ubunge Jimbo la Mpwapwa, Apongeza CCM kwa Ujumuishwaji wa Makundi Maalum

Maiko Salali Arejesha Fomu ya Kugombea Ubunge Jimbo la Mpwapwa, Apongeza CCM kwa Ujumuishwaji wa Makundi Maalum

DWIGHT DANDA KIJANA MDOGO NA MHITIMU WA CHUO KIKUU ATIA NIA UBUNGE KIBAMBA

DWIGHT DANDA KIJANA MDOGO NA MHITIMU WA CHUO KIKUU ATIA NIA UBUNGE KIBAMBA

Katimba aomba ridhaa Ubunge viti maalumu Kigoma

Katimba aomba ridhaa Ubunge viti maalumu Kigoma

SAGAFF AJITOSA KUMRITHI MAVUNDE DODOMA MJINI

SAGAFF AJITOSA KUMRITHI MAVUNDE DODOMA MJINI

Ubalozi wa Marekani waahidi kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Ubalozi wa Marekani waahidi kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.