

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, ameitambulisha rasmi Bungeni Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) na kubainisha kwamba katika kutekeleza majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 itaanza kwa kutoa mafunzo kupitia Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari.
Waziri Kabudi ametoa utambulisho huo tarehe 07 Mei, 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
“Sheria ya Huduma za Habari Sura 229 kwa sasa inaelekeza uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa tayari Bodi hiyo imeishaundwa na ilizinduliwa rasmi tarehe 3 Machi, 2025 na kuanza kufanya kazi. Bodi hii inaongozwa na Mwandishi wa Habari mahiri na mkongwe kwenye tasnia ya habari, Bw. Tido Mhando” amesema Waziri Kabudi.
Waziri Kabudi amesema mbali na majukumu ya msingi ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ambayo ni kusimamia maadili ya waandishi wa habari na weledi wa kitaaluma katika kuandika habari pia itausimamia Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari.
“Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari unalenga kuwezesha mafunzo kwa waandishi wa habari, kusaidia uzalishaji maudhui ya ndani na pia kuwezesha tafiti katika masuala ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma,” amesema Waziri Kabudi.
Amesema ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu hayo yote ikiwemo uzalishaji wa maudhui ya ndani, Mfuko huo chini ya Bodi utaanza kusaidia waandishi wa habari kuwa na vifaa vya kisasa ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kutengeneza maudhui ya ndani.
Waziri Kabudi amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara hiyo itaendelea na majukumu yake ya usimamizi wa Sekta ya Habari ili kuhakikisha inaendelea kukua na kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa na kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na zilizochakatwa kwa weledi wa hali ya juu na waandishi wa habari wenye sifa.
Katika kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa miundombinu ya michezo nchini, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza mchakato wa kuanzisha chombo maalumu cha usimamizi wa miundombinu ya michezo nchini ambacho kitakuwa na mamlaka ya kusimamia uendeshaji, ukarabati na matunzo ya miundombinu yote ya michezo.
“Ni matumaini yetu kwamba kuwapo kwa chombo hiki kutapunguza changamoto za usimamizi wa miundombinu na kutaongeza thamani ya miundombinu ya michezo nchini,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa ili kuimarisha michezo katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara hiyo imeratibu kikao kazi cha mwaka cha Maafisa Michezo Tanzania Bara.
“Kikao hiki kimefanyika sambamba na kikao kazi cha Maafisa Utamaduni nchini kuanzia tarehe 22-26 Aprili 2025 jijini Dar es Salaam, kikao kazi hiki kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya michezo nchini yakiwamo utendaji kazi wa vitengo vya michezo na utamaduni katika ngazi za halmashauri nchini,”ameongeza.
Pia Prof. Kabudi amesema Serikali pia imeendelea na ujenzi wa viwanja vya mazoezi na kupumzikia wananchi ambao unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma ambapo kwa upande wa Dar es Salaam mradi umefikia asilimia 46 na Dodoma mradi huu umefikia asilimia 65.
“Kukamilika kwa mradi huu kutatoa fursa kwa wananchi wa Dar es Salaam, Dodoma na Taifa kwa ujumla kuwa na viwanja vya kutosha vya mazoezi kwa ajili ya michezo mbalimbali ikiwamo, viwanja vya mpira wa mikono, viwanja vya mpira wa miguu, mpira wa wavu, netiboli, mpira wa kikapu, tenisi, na mchezo wa kuogelea.
EVANCE KAMENGE AJITOLEA KUSAIDIA JAMII KAGERA
SERIKALI KUTEKELEZA MFUKO WA UBUNIFU WA SAMIA “SAMIA INNOVATION FUND” WENYE THAMANI YA BIL 2.3
SERIKALI YAENDELEA KUTOA MAFUNZO KWA WALIMU 70,657 UTEKELEZAJI MITAALA ILIYOBORESHWA, YAANZA MAPITIO SHERIA YA ELIMU
DKT. DORIYE AVISHA VYEO VYA KIJESHI MAAFISA 145 NA ASKARI 476 WA NCAA NA KUSISITIZA UCHAPAKAZI, NIDHAMU, MAADILI NA UZALENDO KATIKA ULINZI WA RASILIMALI.
WAHUKUMIWA MIAKA 20 GEREZANI KWA KUHUJUMU MRADI WA ETDCO
Ibraah Afunguka: "Nilifukuzwa Konde Gang na Harmonize"
Watu Wenye Ulemavu Waomba Kuangaliwa kwa Jicho la Kipekee Katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Sekta ya Uvuvi imetoa ajira ya Moja Kwa Moja Kwa Wavuvi 201,661
SERIKALI Imeendelea Kujenga na Kuboresha Miundombinu ya Viwanja vya Ndege
MKURUGENZI WA MASOKO TTB AELEZA FURSA INAYOWEZA KUPATA TANZANIA KUTOKA JAPAN KATIKA ELIMU YA UTALII NA UHIFADHI