Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania? | The Dodoma Post
The Dodoma Post Makala

Zipi Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

Kwa sasa wadau mbalimbali nchini wanatambua kwamba Tanzania ni mwandaaji mwambata wa mashindano ya michezo wa miguu Barani Afrika mwaka 2027 yaani Afcon 2027 kando ya Kenya na Uganda, kila nchi kwa sasa iko kwenye maandalizi yenye kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanyika kwa ustadi na ubora wa hali ya juu.

Thobias Masalu, Gilbert Lyimo
By Thobias Masalu, Gilbert Lyimo
06 Aug 2024
Zipi 	Faida na Fursa za Afcon 2027 Tanzania?

July 5, 2024 Tanzania ilizindua Kamati ya Maandalizi ya Ndani (LOC) ya AFCON 2027, huku ikikabidhiwa majukumu ya kuhakikisha maandalizi yote yanafanyika kwa ufasaha na kwa ufanisi ili kukidhi matakwa yote yanayotakiwa na Shirikisho la Mpira Barani Afrika (CAF) pamoja na lile la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Kamati hiyo ilizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambapo mbali na uzinduzi huo Waziri Mkuu alibainisha fursa na faida za Mashindano hayo makubwa zaidi barani Afrika na kuwarai wadau kuhakikisha wanachangamkia fursa hizo ili waweze kunufaika na mashindano hayo.

“Moja tujiandae kwa kuwa na viwanja, mbili lazima tujiandae kwa utoaji huduma katika sekta nyingine zote, tatu ni lazima tujiandae kuhakikisha kuwa sisi wenyewe watanzania tunanufaika na uwepo wa mashindano haya.”

Pamoja na kwamba serikali imeendelea na maandalizi ya Afcon 2027 ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya uwanjani na ile ya usafiri na usafirishaji lakini kuna maeneo mengi yenye mahitaji ya uwekezaji ambayo yakifanyiwa kazi huenda Afcon 2027 ikawa ya mfano tangu kuanzishwa kwake. Inakadiriwa kuwa mashindano haya yanatarajiwa kutazamwa na zaidi ya watu milioni mia mbili hivyo itasaidia nchi kujitangaza zaidi kimataifa.

“Tumejiandaa kwenye miundombinu ya usafirishaji barabara, njia za reli, maji pamoja na njia ya anga, kuhakikisha kwamba mtu yeyote anayetaka kusafiri kwenda popote anaweza kwenda, lakini pia tumejiimarisha kwenye huduma ya malazi, tunazo hotel zenye hadhi ya nyota tano, nyota nne, zenye hadhi ya kulala wageni wa kimataifa, ziko pande zote mbili na sisi tumejiweka vizuri, usafirishaji wa ndani kama ambavyo mnaona tuna ndege za kisasa na tuna viwanja karibu mikoa yote nchini, bado mikoa mitatu tu na kazi hiyo inaendelea, lakini pia usafirishaji wa njia ya maji, kuunganisha bara na visiwani tuna boti za kutosha tena za kisasa.”

Ni zipi fursa za Kuchangamkiwa na Watanzania?

Kila jambo linapotokea huwa na fursa zake ambazo zikitumiwa na wahusika huzalisha faida kwa kila anayehusika ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, maeneo kadhaa yalibainishwa na Waziri Mkuu Majaliwa kama vile malazi, ujenzi wa viwanja vya mazoezi, sehemu za burudani, uzalishaji bidhaa zenye chapa ya Tanzania.

“Tunawahamasisha kupanga mpango wa uwekezaji, kwenye maeneo ambayo mnadhani tukiwekeza itatuletea faida, lakini pia yatatoa huduma katika eneo hili la kuwapokea wageni wetu, tunahitaji vyombo vya usafiri zaidi kwenye maeneo yote, tunahitaji kuwa na hoteli nyingi zaidi, tunahitaji maeneo ya mapumziko, maandalizi ya maeneo ya mapumziko baada ya kuwa wamecheza wanahitaji kupumzika huduma hizi tunazitarajia kutoka kwenu kwa ujumla mashindano haya ya Afcon kufanyika Tanzania ina masilahi makubwa kwa nchi yetu.”

Inawezekana ukajiuliza ni vipi Mtanzania anaweza kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kama ambavyo serikali inawahamasisha wawekezaji kujitokeza, sasa majibu ya maswali yako yanabainishwa na waziri Mkuu Majaliwa.

“Kupitia mashindano haya pia tutakaribisha uwekezaji mkubwa kufanyika hapa ndani ya nchi uwekezaji huu utakuwa katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji ya mwekezaji mwenyewe leo ukiamua kujenga hoteli nyingine ya nyota tano unaweza kumaliza kabla ya 2027, wale wenye uwezo fanyeni hivyo, Jiji la Dar es Salaam bado halina hotel za kutosha, Arusha bado hoteli hazitoshi, tuna mahitaji makubwa ya hoteli za nyota tano, kwahiyo uwekezaji huu ni mzuri, uwekezaji kwenye sekta ya anga, bado mnakaribishwa, ndege za hapa na pale za mtu mmoja, watu watatu, wanne, watano Watanzania mnayo fursa sasa ya kuwekeza kwenye maeneo hayo.”

Lakini pia akaongeza, “Kuongeza boti za usafirishaji, siyo tu za kwenda Zanzibar hata kwenda Mafia huko Mtwara, Kilwa Kisiwani huko, huu ufukwe wetu wa hapa Dar es Salaam, kutoka Bagamoyo mpaka Temeke hatujaona kama kuna mahali kuna ile michezo ya baharini ambayo pia watu wakicheza mechi wamechoka wataruka tu nyumba tano sita wanaenda kucheza huko nendeni mkawekeze, mashindano hayo yataleta watalii wengi, tuna fursa nzuri za utalii, tuna mbuga za wanyama na aina mbalimbali za wanyama tuna maeneo ya kale yako bara na visiwani, tuna fukwe nzuri zipo, Sadaan huko lakini pia Zanzibar haya ni maeneo ambayo yataleta watalii wengi.”

Faida za Afcon 2027 kwa Tanzania na Watanzania

Ni kama Afcon iko mbali kwa macho ya kawaida lakini kiuhalisia 2027 ni karibu sana na mtu anaweza asione hili kama hatambui kwa namna gani fursa hii ina manufaa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mashindano ya Afcon 2027 kufanyika Tanzania yana maslahi kwa nchi na jamii kwa ujumla kutokana na kwamba yatasisimua maendeleo ya sekta mbalimbali, huku pia yakiipaisha nchi katika medani za kimataifa kimichezo.

“Kwanza yatakuza uchumi, pili yatahamasisha maendeleeo ya michezo yenyewe lakini siyo michezo tu yatahamasisha jamii kwenye maendeleo ya sekta mbalimbali lakini pia kuipatia sifa nchi yetu kwenye michezo, nchi zote duniani zilizopata sifa ya juu kabisa ni kwasababu ziliimarisha sekta ya michezo, sasa tunataka wageuze macho waangazie bara la Afrika na anapofika Afrika aende Tanzania automatically inawezekana, sasa ni lazima tuhakikishe kwamba huduma hizi tunaziimarisha ili tuweze kuzifikia, kwenye kipindi cha miaka miwili  lazima tuhakikishe tunabadilika na tunafika hatua nzuri.”

Machinga ana nafasi katika maandalizi haya?

Pengine mtu mwingine anaweza kuamini kuwa wenye mitaji mikubwa ndo pekee wanaweza kuchangamkia fursa hizo lahasha, kila mmoja anayo nafasi ya kushiriki katika fursa hizi na kubadilisha maisha yake ikiwemo kuongeza kipato chake na taifa kwa ujumla. 

Hivyo serikali inaamini kuwa ni wakati sasa kuhakikisha kila mmoja anayaimba na kuyaishi mashindano hayo kwa kushiriki katika maandalizi yake kuanzia hatua za awali kabisa kama anavyoeleza Waziri Mkuu Majaliwa.

“Mashindano haya yanaweza kutuletea kipato kwa mtu mmoja mmoja, jamii za wanaojishughulisha na biashara, kwahiyo kiuchumi mashindano haya kwetu ni muhimu sana, na sisi tunataka tuone tunaongeza pato la mtu mmoja mmoja kwahiyo tukianza kueleza faida za Afcon tutatoa mianya na kufungua milango kwa mtu mmoja mmoja kuitafuta sekta ambayo ataweza kuisimamia na kufanya maandalizi kwaajili ya kujipatia kipato…

Lakini pia mashindano haya yatachochea biashara, zile ndogo ndogo, za kati na zile kubwa kwahiyo machinga wana nafasi nzuri tu ya kufanya biashara, kuuza bidhaa za kitanzania watu wanataka warudi kwao wakiwa na bidhaa zenye alama ya Tanzania huu ndo wakati wetu.”

Sekta ya Michezo Itaguswa vipi na Afcon 2027?

Mashindano ya Afcon yanahusisha michezo ya mpira wa miguu moja kwa moja unaweza ukajiuliza ni kwa namna gani mashindano haya yataleta chachu ama mabadiliko kwenye eneo la michezo nchini?

Ukweli ni kwamba mashindano hayo yakisimamiwa vyema yataleta chachu kubwa kutokana na kuwa maendeleo ya miundombinu yataimarika nchini kwa kujengwa ama kukarabatiwa viwanja ambavyo vitatumika kuendeleza sekta ya michezo hususani kwa vijana.

“Mashindano haya yatahamasisha vijana wetu kuingia kwenye michezo na wote tunajua michezo sasa ni ajira na ni sekta ambayo inalipa sana kwa sasa, ni sekta ambayo mishahara yao ni mikubwa kuliko hata watumishi wa umma, kwahiyo tunataka tuiendeleze sekta hii ili vijana wengi waende wacheze waajiriwe wapate mafao yao wapate kuendesha familia zao, ni wakati mzuri kuhamasisha vijana wetu kuona kwamba kuingia kwenye michezo ni kuendesha maisha yao, tutumie Afcon kuwapa somo vijana wetu kufungua mianya pengine wachezaji wetu wapate masoko ya kwenda nje ya nchi.” Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha.

Je Mtanzania umejiandaa vipi kuchangamkia fursa hizi? Kazi ni kwako.


 

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Dkt. Ndumbaro: Nitatembelea Mradi Huu Kila Baada ya Wiki Mbili

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027-2

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

MTAALA MPYA WA ELIMU WAANZA KUTUMIKA (MUHAS)

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Safari ya Omary Katanga Barani Afrika na Maandalizi ya Afcon 2027

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi

Afcon 2027 Kuchele, Kamati ya Afcon 2027 Yakabidhiwa Maandalizi